You are currently viewing 38 wafariki ajali ya ndege, 29 wanusurika

38 wafariki ajali ya ndege, 29 wanusurika


Mamlaka ya Anga nchini Kazakhstan imesema watu 38 wamefariki dunia katika ajali ya ndege ya abiria ya kampuni ya Azerbaijan Airlines magharibi mwa nchi hiyo jana Jumatano.

Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Azerbaijan na wengine wamesema kuwa ndege hiyo ilianguka na kuwaka moto karibu na uwanja wa ndege wa Aktau, uliopo pwani ya mashariki ya Bahari ya Caspian. Wameongeza kuwa ndege hiyo ilikuwa na abiria 62 na wahudumu watano.

Shirika la ndege la Azerbaijan Airlines limesema ndege hiyo aina ya Embraer 190, iliyotengenezwa na kampuni ya Brazil ya Embraer, ilijaribu kutua kwa dharura karibu na Aktau.

Mamlaka za Kazakhstan zinasema watu 38 waliokuwa ndani ya ndege wamefariki na wengine 29 wamelazwa hospitalini.

Ripoti zinasema ndege hiyo iliondoka katika mji mkuu wa Azerbaijan, Baku, kuelekea Grozny katika Jamhuri ya Chechen, kusini mwa Urusi, lakini ilibadilisha mwelekeo mara kadhaa kutokana na ukungu.

Vyombo vya habari vya Kazakhstan vinaripoti kuwa kifaa cha kurekodi safari kimepatikana katika eneo la ajali.

Serikali za Kazakhstan na Azerbaijan zinafanya kazi ya kubaini chanzo cha ajali hiyo.

Leave a Reply