You are currently viewing Rais Mwinyi: Sekta binafsi ina mchango kukuza utalii endelevu

Rais Mwinyi: Sekta binafsi ina mchango kukuza utalii endelevu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii hapa nchini katika nyanja tofauti na kusisitiza serikali kuendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuwa na utalii endelevu.

Rais Dk. Mwinyi amesema  hayo alipoifunga ziara maalumu ya mabalozi (safari diplomatic tour) wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini iliolenga kuutangaza utalii wa Tanzania na diplomasia  ya kiuchumi katika nchi zao iliofanyika  hoteli ya  kwanza Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 14 Aprili 2025.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameeleza kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha sekta ya utalii ili kuwa endelevu na kuifanya Zanzibar kuwa kituo muhimu cha utalii kinachotambulika  na kuvutia ulimwenguni.

Amefahamisha kuwa utalii ni sekta muhimu na nguzo ya uchumi wa Zanzibar ambayo mbali na kukuza uchumi sekta hiyo inawaunganisha watu wa mataifa mbalimbali ulimwenguni.

Rais Dk. Mwinyi amesema serikali  imechukua juhudi  kubwa za uimarishaji wa viwanja vya ndege kwa lengo la kutoa huduma bora kwa watalii ,upanuzi wa miundombinu ya barabara  pamoja na huduma za afya,umeme na upatikanaji wa maji ni hatua muhimu za kufanikisha  kuwa na utalii unaovutia na  endelevu.

Amebainisha kuwa kuchukua hatua hizo nchi imekuwa ikipokea idadi kubwa ya watalii kila mwaka wanaofikia takribani milioni mbili na kuiunganisha Zanzibar na mashirika ya kimataifa ya ndege 34 yanayoleta watalii hapa nchini

Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameielezea Filamu ya Royal Tour ya Rais Samia Suluhu Hassan na ziara yake kuwa ni nyenzo muhimu zilivyovitangaza vivutio vya utalii wa Tanzania kwa mafanikio ulimwenguni.

Rais Dk. Mwinyi amesema mikakati ya uwekezaji imewezesha kupokea watalii 548,503 mwaka 2022 na mwaka 2023 imepokea wageni 736,755 na kutunukiwa tuzo  ya World Travel Award kwa kuwa kituo kinachoongoza kwa matamasha na mikusanyiko ya  kimataifa.

Akizungumzia Safari Diplomatic Tour amesema ni hatua muhimu ya ushirikiano miongoni mwa mataifa kupitia sekta ya utalii na  kuwaomba mabalozi hao kuwahamasisha wawekezaji wa nchi hizo kuwekeza nchini kwani bado fursa za uwekezaji ni nyingi hususan utalii wa mikutano na matamasha.

Mabalozi wa Mataifa takribani 34 wanaoziwakilisha nchi zao tanzania walikuwa na ziara  maalum ya  kuvitembelea vivutio vya utalii Arusha  Ngorongoro na Zanzibar ili hatimaye kuvitangaza katika nchi zao.

Ziara hiyo imeandaliwa na Wizara ya Utalii na Mali Asili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar na  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Leave a Reply