You are currently viewing Leo XIV kutoka Marekani ndiye Papa mpya

Leo XIV kutoka Marekani ndiye Papa mpya

Kadinali Robert Prevost ametangazwa kuwa Papa mpya. Papa Robert Prevost atajulikana kama Papa Leo XIV.

Kardinali Prevost ni mzaliwa wa Chicago nchini Marekani ambaye hadi anchaguliwa leo tarehe 8 Mei 2025, alikuwa akihudumu kama mkuu wa Dicastery wa kanisa kwa Maaskofu.

Papa Leo XIV mwenye umri wa miaka 69 ametumia muda wake mwingi akitumikia nchini Peru na ana uraia wa Marekani na Peru.

Akihutubia umati uliokuwa ukishangilia kwa Kiitaliano, Papa Leo XIV alisema: “Amani iwe nanyi nyote.

“Wapendwa, ndugu zangu, hii ni salamu ya kwanza ya ufufuko wa Kristo. Ningependa kutoa salamu ya amani iwafikie familia zenu, ninyi nyote, popote mlipo. Amani iwe nanyi.”

Alitoa shukrani zake kwa mtangulizi wake, Papa Francis, huku akisema anataka kuwasilisha baraka zake kwa watu kama Papa Francis alivyofanya mara ya mwisho alipojitokeza katika uwanja wa St Peter’s Square.

“Ubinadamu unahitaji Kristo kama daraja la kufikiwa na Mungu na upendo wake. Tusaidie, na tusaidiane, kujenga madaraja.”

Papa Leo XIV amesema hayo kisha aliwashukuru makadinali waliomchagua wakati wa mkutano huo wa siku mbili.

“Sote tunaweza kutembea pamoja kuelekea nyumba ya Mungu ambayo ametuandalia,” alisema. “Salamu maalum kwa Kanisa la Roma.”

Kisha Provost alianza kuzungumza kwa Kihispania ili kushukuru dayosisi yake ya zamani huko Peru “ambapo watu waaminifu walishiriki naye imani na kujitoa kwa mengi”.

Lakini wengi wanajiuliza Robert Francis Prevost ni nani. Huyu alikuwa kiongozi wa Dikasteri ya Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini tangu mwaka 2023. 

Kabla ya hapo alihudumu kama Askofu wa Chiclayo nchini Peru kutoka 2015 hadi 2023. Kabla ya kuwa Askofu wa Chiclayo alikuwa mkuu wa shirika la Mtakatifu Agustino (Order of St.Augustine) kutoka mwaka 2001 hadi 2013.

Amezaliwa mwaka 1955 huko Chicago, Illinois nchini Marekani. Ni msomi mwenye degree 5. Alipata daraja takatifu la Upadri mwaka 1982 baada ya kuhitimu shahada ya Falsafa (Bachelor degree in Philosphy) na Shahada ya Theolojia (Bachelor degree in theology) huko Illinois, Calfornia. Mwaka 1984 alitumwa masomoni nchini Italia na kuhitimu shahada ya kwanza ya sheria za Kanisa katika Chuo kikuu cha Mtakatifu Thomas wa Aquinos kilichopo Rome.

Mwaka 1987 alihitimu Shahada ya umahiri katika sheria za Kanisa (Juris Canonici Licentiatus) na baadae Shahada ya uzamivu katika sheria za Kanisa (Juris Canonici Doctor) kutoka Pontifical College of St. Thomas Aquinas.

Kisha alirudi Marekani na kutumwa umisheni huko Amerika ya kusini ambapo alitumikia nafasi mbalimbali ikiwemo Askofu wa jimbo la Chiclayo nchini Peru. Mwaka 2015 aliomba na kupewa uraia wa Peru. Leo Mei 8, 2025, amechaguliwa kuwa Papa wa 267 akimridhi Papa Francis, na amechagua kutumia jina Leo XIV. Papa Leo XIV anakua Papa wa kwanza mzaliwa wa Amerika Kaskazini.!

Leave a Reply