You are currently viewing Samia kukomesha migogoro wakulima, wafugaji Kilosa

Samia kukomesha migogoro wakulima, wafugaji Kilosa

Mgombea wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amesema atakapochaguliwa kuiongoza Tanzania kwa miaka mitano ijayo, atahakikisha programu ya Tutunzane inatekelezwa hadi wilayani Kilosa mkoani Morogoro.

Dkt Samia ameyasema hayo leo, Jumamosi, Agosti 30, 2025 alipozungumza na maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Kilosa waliojitokeza katika mkutano wake wa kampeni za urais zinazoendela hadi Oktoba 27, 2025.

Amesema programu hiyo imeonyesha mafanikio makubwa wilayani Mvomero mkoani humo, kwa kuwezesha

wakulima na wafugaji kuishi kwa amani na upendo, baada ya migogoro ya muda mrefu.

“Tutaileta programu hiyo hapa. Lakini kubwa Zaidi ni kuongeza maeneo ya wafugaji, kuna maeneo yanayopata ekari milioni 3.46 na tunakwenda kuongeza hadi milioni 6 kwa ajili ya wafugaji. Hii ni kuepusha migogoro ya wakulima na wafugaji,” amesema Dkt Samia.

Sambamba na hayo, ameahidi kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Idete wilayani Kilosa mkoani Morogoro, ili litumike kwa ajili ya kutoa huduma ya maji kwa wananchi, pia shughuli za kilimo cha umwagiliaji na kuzalisha kwa tija zaidi.

Pia, ameahidi kujenga soko la kisasa wilayani humo, kama ilivyofanyika katika maeneo mengine nchini.

Leave a Reply