Rais Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa wananchi baada ya kukabiliwa na uhaba wa maji, akisema umesababishwa na upungufu wa mvua katika kipindi cha miezi saba ya mwaka 2025 uliochochea kuwepo kwa ukame.
Katika kukabiliana na hali hiyo hususan kwa Dar es Salaam, amesema Serikali ilihakikisha vyanzo vyote vya maji vilivyo karibu vinaelekeza maji jijini humo na kufufua visima vilivyokuwa havifanyi kazi.
Aidha, amesema mvua zinazoendelea kunyesha ndani ya Desemba zinaongeza kina cha maji kwenye vyanzo vya Ruvu Juu na Ruvu Chini na zinarejesha hali nzuri ya upatikanaji wa maji.
Amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa Bwawa la Kidunda na awamu ya pili ya mradi wa maji wa Kimbiji Mpera ili kuondosha kabisa shida ya maji Dar es Salaam na mikoa jirani, hata katika hali ya ukame.
Rais Samia ameeleza hayo leo, Jumatano Desemba 31, 2025 katika hotuba yake kwa Taifa aliyoitoa akiwa Ikulu Ndogo ya Tunguu iliyopo Mkoa wa Kusini Unguja visiwani Zanzibar.
