Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amesema uamuzi wa Serikali kujenga Taasisi ya Sayansi za Bahari (UDSM-IMS) visiwani Zanzibar, umelenga kuchochea ajira na kuufikia uchumi jumuishi.
Ametaka wananchi wanaoishi maeneo ya karibu na taasisi hiyo na wanaojishughulisha na masuala ya bahari wanufaike kwa kuanzishwa mafunzo ya muda mfupi kwa ajili yao.
Dkt Samia ametoa kauli hiyo leo, Alhamisi Januari 8, 2025 katika hotuba yake, wakati wa uzinduzi wa majengo ya IMS, Buyu visiwani Zanzibar.
Ameeleza tafiti na maarifa yatakayozalishwa chuoni hapo, yatasaidia uamuzi wa kisera unaolinda rasilimali za bahari sambamba na kuongeza tija na kipato cha wananchi kwa kizazi cha sasa na baadaye
Amesema maendeleo ya taasisi ya sayansi za bahari yanapaswa kuinufaisha na jamii inayozunguka kupitia ajira, huduma, biashara na shughuli za kijamii zitakazochangia kipato.
Ametaka taasisi hiyo kuanzisha mafunzo mafupi ya vitendo hususan kwa wanaoishi karibu ili waongeze tija, kipato na uelewa wa matumizi endelebvu ya rasilimali za bahari.
