Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan amesema amani, usalama na utulivu wa kisiasa ni miongoni mwa mambo yanayokuza uwekezaji nchini, huku akiwaonya wanaotaka kuiharibu.
Dkt Samia ameeleza leo Alhamisi Januari 9,2025 wakati akizindua hoteli ya kisasa ya Jaz Elite Aurora iliyopo, Michamvi Mkoa wa Kusini Unguja Zanzibar. Uzinduzi huo ni sehemu ya shamrashamra ya kusheherekea miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Dkt Samia ameeleza kuna kuna wawekezaji wapo wengi wanaovutiwa na hali ya amani na utulivu iliyopo Tanzania, hivyo amewataka wanaotaka kuichokonoa kuacha mara moja.
“Acheni mara moja, amani ikichafuka haichagui. Tuulizeni sisi wa upande wa pili (Tanzania Bara), amani ilipochafuka pale Dar es Salaam tu… nenda kaulize vijana kama leo wanataka kuingia barabarani, hakuna anayetamani,”

“Kwa hiyo amani ikivunjika haichagui niwaombe sana, maendeleo yetu, kunawiri kwetu, kulala na kuamka salama, tuitunze amani ya nchi yetu.Tofauti za mawazo zipo, lakini zisitugawe wala kuharibu utulivu wa kisiasa na amani yetu,” ameeleza Dk Samia.
Aidha Dkt Samia amewaahidi wawekezaji wa Tanzania Bara na Zanzibar, kuwa Serikali zote mbili zitaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuwavutia zaidi.
