Majukumu ya kuiongoza nchi, hayakumzuia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutenga muda wa kuangalia mechi za timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars.’
Hata hivyo, kuangalia ni jambo moja, lakini huruma na hofu aliyokuwa akipitia kila ilipotokea mchezaji wa Taifa Stars amefanyiwa madhambi na mpinzani, ilikuwa hatua ngumu kwake.
“Siku hiyo nilikuwa nimefunga (ibada), wakati naendelea na futari zangu tayari mchezo unataka kuanza. Nikakaa nikaangalia watoto wangu (Timu ya Taifa Stars) kazi waliyoifanya.
“Lakini, nimeondoka pale mwili wote unaniuma, maana wakipigwa wakizuiwa mimi eeee… eee…. wakiwekewa miguu wakisukumwa mimi Mungu wangu wee… mbona wataniumizia watoto. Nimeondoka pale mwili unaniuma, lakini hongereni sana, mmefanya kazi nzuri sana,” amesema Dkt Samia.
Katika michuano hiyo iliyoanza Desemba 21, 2025, Tanzania ilipangwa katika kundi C lililohusisha mataifa ya Nigeria, Tunisia na Uganda.
Hata hivyo, Tanzania ilifuzu hatua ya 16, baada ya kushika nafasi ya tatu katika kundi hilo. Hatua iliyoiwezesha kuweka rekodi tangu ianze kushiriki michuano hiyo mikubwa Afrika.
