Siku ya leo, 28 Januari 2026, shirika la ndege la Air Tanzania limezindua rasmi safari mpya za moja kwa moja kwenda Accra, Ghana, kupitia Lagos, Nigeria.
Safari hizi zitakuwa zikifanyika mara tatu kwa wiki, katika siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.
Uzinduzi huu unalenga kuimarisha utalii, kurahisisha usafiri na kukuza uchumi kati ya Afrika Mashariki na Magharibi, sambamba na kuendeleza uhusiano wa kihistoria, kiutamaduni na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi za Afrika Magharibi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Air Tanzania, Mhandisi Peter Ulanga, amesema safari hizi ni ndoto ya muda mrefu iliyotimia, na zitaleta fursa kwa mashabiki wa soka kusafiri na kuunga mkono timu zao katika michuano ya Afcon inayotarajiwa kufanyika mwaka 2027.
Aliongeza kuwa shirika limeongeza idadi ya ndege zake kutoka tisa mwaka 2021 hadi 16 sasa, huku idadi ya vituo vya safari ikiongezeka kutoka 24 hadi 32 ndani ya miezi 15.
