Kanisa Katoliki nchini limepata pigo kufuatia kifo cha Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo, kilichotokea jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Yude Thaddeus Ruwai’chi, Kardinali Pengo alifariki dunia saa 4:00 usiku wa kuamkia leo Ijumaa, Februari 20, 2026, alipokuwa akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Taarifa ya kifo chake ilitolewa rasmi usiku wa kuamkia leo, huku Kanisa likiwa katika maombolezo kufuatia kuondokewa na kiongozi huyo aliyewahi kulitumikia Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwa miaka mingi.
Askofu Mkuu Ruwai’chi amesema utaratibu wa mazishi na ratiba ya kuaga mwili wa marehemu zitatangazwa baadaye.
