Na Mwandishi Wetu, Singida
Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umezindua awamu ya kwanza ya mpango wa hedhi salama mashuleni unaojulikana ‘Msaidie Binti Abaki Shule’ unaolenga kuwawezesha wasichana, hususan wanaoishi vijijini kuhudhuria masomo muda wote, hivyo kuongeza ufaulu wao darasani kwa kuwapatia misaada mbalimbali ikiwemo taulo za kike.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo kupitia mpango kwa shule za Msingi na Sekondari hapa nchini, Meneja wa Uwezeshaji na Uwajibikaji kwa Jamii wa EACOP, Bi. Clare Haule alisema mpango huo utaanza kutekelezwa katika mikoa mitatu ya Singida, Shinyanga na Dodoma, ukihusisha jumla ya shule 19 na kunufaisha zaidi ya wanafunzi 4,596.

Alisema kuwa katika awamu ya kwanza, mpango huo utatekelezwa katika shule sita zilizopo mkoani Singida, saba mkoani Shinyanga na sita katika mkoa wa Dodoma.
“Mpango huu utaenda kwa awamu, na awamu hii ya kwanza tumeanza katika mikoa hiyo mitatu tu na kuendelea katika mikoa mingine hapa nchini,”
“Kwa ujumla tunatarajia kuwafikia wanafunzi 4,596 katika shule 19,” alisema Haule.
EACOP inatekeleza mpango huu kama sehemu ya mpango wake wa kuwekeza kiuchumi na kurudisha kwa jamii (SEI/CSR) kwa waguswa wanaoishi katika maeneo unapopita mradi huo katika mikoa nane hapa nchini.
Aliongeza kuwa tafiti mbalimbali bado zinaonyesha kuwa asilimia 15 hadi 20 ya wasichana hukosa masomo kwa siku moja hadi mbili kila mwezi kutokana na hedhi, hali inayosababishwa na ukosefu wa huduma nzuri za kujistiri shuleni pindi wanapokuwa katika hedhi na ukosefu wa taulo za kike.

Haule alisema kupitia mpango huo, EACOP inalenga kutoa elimu ya afya ya uzazi na kuweka mazingira ya hedhi salama kwa wanafunzi hao ili kupunguza changamoto ya uto ro na ufaulu hafifu kwa wanafunzi wa kike .
Aidha, alibainisha kuwa mbali na mpango huo, mradi wa EACOP unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii kwa lengo la kuboresha ustawi wa wananchi walioguswa na mradi huo, ikiwemo miradi ya kilimo, ufugaji wa nyuki, pamoja na mafunzo ya ujasiriamali na biashara.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Victorina Ludovick, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa katika uzinduzi huo , mpango huo unaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayosisitiza usawa wa kijinsia na upatikanaji wa mahitaji muhimu kwa watoto wakiwemo wa kike.
“Kwa kusaidia usimamizi wa afya ya hedhi salama shuleni tunajenga msingi wa wanawake bora na wenye uwajibikaji kwa taifa letu,” alisema Dkt. Victorina.
Alisisitiza kuwa ipo haja ya kuwalinda na kuwawezesha wasichana, ambao ni tegemeo la maendeleo ya taifa, kwa kuwapatia mazingira salama ya kujifunzia ili waweze kuendelea na masomo yao bila vikwazo.
Naye Kaimu Afisa Elimu wa Mkoa wa Singida, Bi.Regina Yaghambe, alisema mpango huo umekuja wakati muafaka kwani utasaidia kupunguza utoro miongoni mwa wasichana unaotokana na changamoto za ukosefu wa mazingira ya hedhi salama kwa wasichana waliopo shuleni.
Baadhi ya wazazi waliohudhuria uzinduzi huo walisema kabla ya mpango huo, watoto wao walikuwa wakikosa masomo wanapokuwa katika hedhi kutokana na ukosefu wa mahitaji muhimu ikiwemo taulo za kike na sehemu za kujistiri.
Waliongeza kuwa wakati mwingine walilazimika kuwapatia watoto wao vipande vya nguo ili kujistiri, huku wengine wakitumia hata majani ya mimea kutokana na ukosefu wa taulo za kike , unaosababishwa wakati mwingine na kipato kidogo kwa baadhi ya wazazi/ walezi na ukosefu wa taulo hizo katika baadhi ya maeneo, hasa vijijini.
“Tunashukuru EACOP kwa kuanzisha mpango huu kwa ajili ya wasichana wetu waliokuwa wanakosa masomo na kuhisi kutengwa na wenzao. Huu ni msaada mkubwa sana kwetu unaoleta motisha ya ufaulu na kujiamini kwa wasichana shuleni,” alisema Bi.Faulina Sinde, mkazi wa Igauli.
Kwa upande wao, wanafunzi waliopatiwa taulo hizo walisema msaada huo utawasaidia kuongeza kujiamini wanapokuwa katika hedhi na hivyo kuweza kuhudhuria vipindi vyote vya masomo.
Mmoja wa wanafunzi hao, Edina Metusaeli anayesoma kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Ntonge, alisema msaada huo utawawezesha kuhudhuria masomo bila kukosa vipindi kama ilivyokuwa hapo awali.
“Taulo hizi zitatusaidia kuhudhuria vipindi vyote bila kukosa na kutuwezesha kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zetu,” alisema.
Uzinduzi wa mpango huo umefanyika katika Shule ya Sekondari Igauli iliyopo katika Kijiji cha Igauli, Kata ya Ntonge, Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Mradi wa EACOP wenye urefu wa kilomita 1,443 unaanzia Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, mkoani Tanga .
Wanahisa wa mradi huo ni kampuni ya TotalEnergies inayomiliki asilimia 62 ya hisa, wakati Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Shirika la Mafuta la Uganda (UNOC) kila moja yakimiliki asilimia 15, huku kampuni ya mafuta ya China (CNOOC), ikimiliki asilimia 8 ya hisa za mradi huo.
