You are currently viewing CCBRT yarejesha furaha kwa wenye matatizo ya macho Dar

CCBRT yarejesha furaha kwa wenye matatizo ya macho Dar

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Hospitali ya CCBRT imeendelea kutoa huduma ya macho na ushauri nasaha kwa wakazi wa Dar es Salaam katika Kituo cha Afya cha Anglikana kilichopo Buguruni, Manispaa ya Ilala kwa siku mbili mfululizo ikiwa ni sehemu ya kuwapa furaha wale wote wenye matatizo ya macho.

Akizungumza kwa nyakati tofauti pembezoni mwa zoezi la upimaji macho, Afisa Mkuu wa Maendeleo ya Jamii na Utafiti, Bi. Rhoda Ndakwe amesema zoezi hilo ni endelevu na kwamba linafanyika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani na Kwaresma.

Muuguzi kutoka Hospitali ya CCBRT, Bi.  Gloria Machange, akimpima presha ya macho mmoja wa wananchi waliojitokeza kwenye kambi ya siku mbili ya upimaji macho inayotolewa bure kwenye kituo cha Afya cha Anglikana.

“CCBRT imejiwekea utaratibu wake kutoa huduma ya macho na ushauri ili kusaidia jamii kukabiliana na matatizo ya macho,” Alisema Bi. Rhoda kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo Bi.  Brenda Msangi.

 Amesema zoezi hilo la upimaji macho na utoaji ushauri nasaa bure limefanywa na hospitali hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Christian Blind Mission (CBM) limepata mafanikio makubwa kutokana na watu wengi kujitokeza kupima macho.

“Huduma hii  inatolewa bure na itaendelea  katika  Wilaya nyingine  zote  za mkoa wa  Dar es Salaam zikiwemo Temeke, Kigamboni, Kinondoni na Ubungo pia,” alisema Bi. Rhoda.

Akielezea zaidi kuhusu zoezi hilo Bi. Rhoda amesema CCBRT imekuwa ikitoa huduma hizo bure sehemu mbalimbali hapa nchini kwa kushirikiana na wafadhili mbalimbali wakiwemo CBM, Light For The World (LFTW).

Mratibu kutoka Hospitali ya CCBRT, Bi.  Mariam Mchomvu, akifafanua jambo kwa wananchi waliojitokeza kupata huduma ya upimaji macho na ushauri nasaha inayotolewa bure,ambayo iliyofanyika siku mbili katika kituo cha Afya cha Anglikana kilichopo Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam jana.

“CCBRT kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inalenga kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya rika tofauti katika jamii yetu, kuhakikisha kila mtu anapata huduma muhimu za macho. Ndiyo maana tukaweka kambi ya siku mbili   ili wakazi wa Ilala wapate huduma hii,” Alisema Bi. Rhoda.

Hospitali ya CCBRT ni miongoni mwa hospitali chachen hapa nchini zinazotoa pia huduma mbalimbali  za kibobezi zikiwemo   Huduma za macho, huduma za  figo na usafishaji Figo, huduma za mifupa, Huduma za uzazi na magonjwa ya wanawake, huduma za  upasuaji pamoja  radiolojia  na nyingine nyingi.

Leave a Reply