Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Serikali kupitia Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) imesema ipo mbioni kuanzisha Kituo cha Kimataifa cha Kuduma za kifedha ( IFC) hapa nchini ili kuvutia uwekezaji wa fedha na mitaji kwa ajili ya kukuza na kuchochea uchumi.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi kazi cha fedha cha TNBC, Dk. Natu El Maamry Mwamba katika kikao kazi cha kikundi hicho kinachohusisha wajumbe kutoka sekta ya umma na sekta binafsi.
Amesema uanzishwaji wa kituo hicho kwa sasa upo katika hatua ya awali ya uwasilishwaji wake kwa wajumbe wa baraza hilo chini ya TNBC, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya uanzishwaji wake.
“Kituo hicho kitakuwa na mambo yote muhimu na kuainisha maeneo ambayo wawekezaji wanaweza kuweka mitaji yao katika maeneo mbalimbali ikiwemo madini na gesi,” amesema.
Amesema hatua hiyo pia itawawezesha wawekezaji wa ndani kupata mitaji kama inavyofanywa na baadhi ya makampuni ya kigeni yanayotumia mitaji kutoka nchi za nje kwa ajili ya uwekezaji wao hapa.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Natu amesema kuwa taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo zipo tayari kulifanyia kazi na kuliharakisha jambo hilo kwa kushirikiana na wadau wengine, hatua ambayo itasaidia Tanzania kukua kiuchumi na kutumia rasilimali zake kuwa kituo kikubwa cha uwekezaji na kuchangia ukuaji wa uchumi.
“Tayari kamati inayohusika na maandalizi ya uanzishwaji wa kituo hicho iliyoundwa na TNBC kwa kuhusisha wadau kutoka sekta mbalimbali imeshatoa mapendekezo ya hatua zinazotakiwa kufuatwa, ikiwemo serikali kutoa tangazo maalumu la uanzishwaji wa kituo hicho katika gazeti la serikali na kuchagua eneo kitakapojengwa kituo hicho,” alisisitiza.
Dk. Natu amesema kamati hiyo imependekeza kuanzishwa kwa sheria, kanuni na miongozo itakayoratibiwa utendaji kituo hicho.
“Kupitia kituo kama hicho, nchi kadhaa duniani zimepiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika uwekezaji, ikiwemo nchi ya Rwanda, ambayo ni ya tatu Afrika kwa kuwa na kituo bora ambacho tayari kimechangia takribani ajira 50,000 katika nchi hiyo ndogo barani Afrika na kujiingizia kiasi kikubwa cha fedha.,” amesema.
Mwenyekiti huyo wa kamati aliitaja piq Kenya kama nchi nyingine inayofanya vizuri, licha ya kuanzisha kituo hicho katika miaka ya hivi karibuni na kuchangia takriban ajira 26,000, huku kituo hicho kikiwa ni sehemu ya malengo ya Dira ya 2050 katika kukuza uchumi wa nchi hiyo.
Nchi zilizopiga hatua ya maendeleo ya kiuchumi kwa kuwa na vituo hivyo ni pamoja na Marekani, Uingereza, Dubai, HongKong na Malaysia.

Hata hivyo, licha ya kuchelewa utekelezaji wake, imeelezwa kuwa Tanzania ina nafasi nzuri sana ya kuvutia uwekezaji wa mitaji ukilinganisha na nchi nyingine za jirani kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo za kijiografia, uwepo wa rasilimali mbalimbali kama vile madini na gesi ambazo zinavutia uwekekezaji na mazingira tulivu ya kufanya biashara yanayochangiwa na uwepo wa amani na utulivu.
Mapendekezo hayo yametoa maoni ya kituo hicho kujengwa katika jiji la Dar es Salaam kwa kuwa kitovu kikuu cha biashara hapa nchini, huku jiji hilola kibiashara likitajwa kuwa na wawekezaji, wafanyabiashara wengi na taasisi mbalimbali za kifedha.
Naye Katibu Mtendaji wa TNBC Dkt. Godwill Wanga amesema kuwa kikao hicho kimetoka na maazimio mbalimbali, ikiwemo kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuvutia wawekezaji, uwepo wa bima ya afya kwa Watanzania na bima ya mazao kama sehemu ya kukuza uchumi.
Lakini pia kupitia maboresho ya kodi kupitia Tume ya Rais ili kuondoa kero kwa wafanyabiashara na kuvutia uwekezaji zaidi.
“Kikao hiki piakimeweka mikakati ya kuwashawishi Watanzania kuwekeza katika hati fungani na kuangalia namna ya kuweka mazingira mazuri ya ushawishi kwa wawekezaji pindi kituo hicho kitakapoanzishwa ili kuwapa imani zaidi wawekezaji hao na mitaji yao,” alisema Dk. Wanga.
Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kimeagiza utolewaji wa Jamii Namba ( namba ya utambuzi) kwa kila mtu ili kuhamasisha ulipaji kodi na kutanua wigo wa mapato kwa ajili ya maendeleo ya nchi na kutoa elimu ya kuhamasisha sekta ya umma na sekta binafsi ya kutoa elimu ya uwekezaji kwa Watanzania.
Naye Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Bw Vicent Minja ambaye ni mjumbe wa kikundi kazi hicho akiwakilisha sekta binafsi amesema kuwa wameainisha mapendekezo mbalimbali, ikiwemo kuboresha mazingira ya kufanya biashara ili kuongeza na kuvutia uwekezaji na kutaka kituo hicho kuwa na taratibu ambazo hazitaingiliwa na Serikali, kama kinavyofanya kituo cha IFC cha Dubai ili kutoa imani kwa wawekezaji na mitaji yao.
Mapendekezo mengine yaliyotolewa ni kuhamasisha wafanyabiashara wa ndani kutumia soko la mitaji ili kushiriki moja kwa moja katika uwekezaji.
Aidha, mjumbe wa mkutano huo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi nchini (PPPC), Bw. David Kafulila aliitoa wazo la kualikwa kwa wataalamu wa Soko la Mitaji la Dar es Salaam (DSE) katika kikao kijacho cha kikundi kazi hicho ili kutoa elimu hiyo kwa wajumbe wa kikundi kazi hicho.
