You are currently viewing Kampeni ya ‘Mjue Jirani Yako’ yashika kasi Magu, wanafunzi wanolewa kuhusu uhamiaji

Kampeni ya ‘Mjue Jirani Yako’ yashika kasi Magu, wanafunzi wanolewa kuhusu uhamiaji

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

KATIKA kutimiza lengo la kuishirikisha jamii kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu uhamiaji, Idara ya Uhamiaji wilayani Magu imezindua klabu za uhamiaji shuleni kwa lengo la kuwajengea uelewa wanafunzi kuhusu usalama wa namna wanavyopaswa kuwa wazalendo na walinzi kwa kuwafichua wahamiaji haramu.

Uzinduzi huo umefanyika jana Jumatano katika shule ya Msingi Mugini iliyopo wilayani Magu ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa kampeni ya ‘Mjue Jirani Yako’ ambayo pia inalenga kusaidia kushirikisha jamii kulinda amani na kufichua wahamiaji haramu.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Naibu Kamishna wa uhamiaji wa mkoa, Dominick Kibuga amesema ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya uhamiaji umekuwa nguzo muhimu  katika kuleta tija  ya kulinda usalama wa Taifa.

Amesema uanzishwaji wa klabu za uhamiaji katika shule na vyuo umelenga kuwajengea wanafunzi uzalendo na uelewa wa kupambana na uhamiaji haramu sehemu mbalimbali nchini.

Awali akizindua klabu hiyo Mkuu wa wilaya ya Magu, Jubilate Lauo amesema kuwapa wanafunzi elimu ya uhamiaji ni jambo la muhimu katika karne hii kwani itawasaidia kujifunza mambo ya uhamiaji na kujijengea uzalendo na uwajibika wa kama watoto wa Tanzania.

“Elimu hii inawajengea watoto kuelewa mipaka ya nchi na umuhimu wa kufuata sheria za nchi na kujijengea tabia ya uwajibika wanapokuwa watu wazima. Mtoto atakuwa mlinzi namba moja katika mazingira anayotokea.

Naye Afisa uhamiaji wilaya ya Magu na Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiajii, Salma Katongo amesema jamii inapaswa kuelewa mambo mtambuka kuhusu uhamiaji hivyo kupitia kampeni ya ‘Mjue Jirani yako’ jamii inashirikishwa katika dhana nzima ya ulinzi na usalama wa nchi.

“Tunasisitia hili kwani kutokana na ukamataji wetu hawa wahamiaji haramu wanahifadhiwa au kufanyishwa kazi na jamii ndio maana tukaona tukishirikisha jamii itatusaidia katika utendaji wetu wa kazi,” amesema.

Nao baadhi ya wanafunzi wanaounda Klabu hiyo, Joan Jonathan na Deni Katunzi wamesema klabu hiyo itawasaidia kufahamu masuala mbalimbali ya uhamiaji, pia kumtambua raia wa Tanzania na kumjua mhamiaji ni nani.