Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, amesema biashara ya Tanzania na Rwanda imekua na kufikia Sh644 bilioni mwaka jana, huku uwekezaji nao ukiimarika kati ya pande hizo.
Mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo, Jumapili Mei 3, 2026 alipozungumza na waandishi wa habari, baada ya kikao chake cha uwili na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, aliyefanya ziara ya siku moja nchini.
Amesema kuanzia mwaka 1997 hadi Machi 2026 Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania imesajili miradi 42 ya uwekezaji kutoka Rwanda yenye thamani ya Dola za Marekani 325.5 milioni (zaidi ya Sh813.7 bilioni).
Kwa mujibu wa Dkt Samia, miradi hiyo imezalisha jumla ya ajira 2,225 kwa Watanzania.
“Licha ya kwanza takwimu hizo zinatia moyo kwenye biashara yetu, tumekubaliana kuendelea kushirikiana ili kukuza uwekezaji, hususan kwenye kuondoa vikwazo vya kikodi, tuzungumze tuviondoe ili tunufaike na masoko ya kikanda chini ya EAC na Mkataba wa Biashara Huria wa Afrika (AfCFTA),” amesema.
