HALMASHAURI ya Wilaya ya Magu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwamo Jeshi la polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Chuo cha udereva Tabora, wametoa mafunzo ya usalama kwa madereva bodaboda zaidi ya 700 wa wilaya hiyo ili kuwawezesha kufahamu sheria na kuzitii na kujiepusha na uhalifu.
Pia mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha madereva hao kurasimisha kazi yao, ikiwamo kupata cheti, leseni huku taasisi mbalimbali za serikali ikiwamo NIDA, RITA na NSSF zikiwawezesha kupata vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho vya Taifa na kujiunga na mfuko wa hifadhi ya jamii.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika Mjini Magu, Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Zuberi Said Zuberi amesema msukumo wa mafunzo hayo umetokana na kundi kubwa la madereva bodaboda kutokuwa na nyaraka muhimu za utambulisho hali inayowakwamisha kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali na wadau wengine.

Zuberi ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya uhakiki wa mikopo ya asilimia inayotolewa na halmashauri ya wilaya ya Magu, amesema changamoto kubwa waliyoibaini ni maafisa usafirishaji (madereva bodaboda) wengi kutokuwa na leseni wala vyeti.
“Hivyo tumeona ni jambo jema kuwapatia mafunzo ili kupata vyeti na leseni lakini pia kupata viambatanisho vingine kama vyeti vya kuzaliwa, utaifa na vingine. Hili ni jambo jema kwa maisha yetu ya leo na ya baadae,” amesema.
Aidha, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Edward Kihamba amewataka madereva hao kuipenda na kuithamini kazi yao huku akisisitiza halmashauri inawatambua na hakuna atakayewatweza.
Naye Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Diana Philemon amesema maafisa usafirishaji ni kundi muhimu hivyo lazima wajilinde wenyewe kwa kujiepusha kushirikiana na watu waovu lakini pia kutoa ushirikiano kwa serikali pale inapowahitaji.
Wakati Mwenyekiti wa umoja wa madereva bodaboda hao, Phinias Eliya ameishukuru halmashauri kwa mafunzo hayo, kuwajali na kulitambua kundi hilo kubwa kwa maendeleo ya jamii.
“Program hizi za mafunzo zitakuwa msaada mkubwa kwetu kwa sababu Magu pekee kwenye umoja wetu tunao wanachama zaidi ya 6800 ambao wamegawanyika kwenye kanda sita, vituo 138 vinavyounda umoja wetu,” amesema.
