You are currently viewing Wabunge: Hakuna ubaguzi wa dini, Tanzania ina uwezo kushughulikia changamoto za ndani

Wabunge: Hakuna ubaguzi wa dini, Tanzania ina uwezo kushughulikia changamoto za ndani

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Baadhi ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamesema Tanzania hakuna ubaguzi wa dini, huku wakitayataka mataifa ya nje kuliheshimu Taifa hili ambalo linaweza kushughulikia changamoto zake za ndani.

Kauli za wawakilishi wa wananchi zinaunga mkono kile kilichosemwa asubuhi na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), kwamba Tanzania hakuna ubaguzi wa dini na viongozi dini mbalimbali wanaishi katika misingi ya amani, utulivu na upendo.

Chimbuko la suala hilo ni muswada uliowasilishwa kwenye Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje Marekani na maseneta wawili wanaotaka wanapendekeza Marekani kufanya tathmini mpya ya ushirikiano wa masuala mbalimbali ikiwemo ya kiusalama, kiuchumi na kidiplomasia baina ya taifa hilo na Tanzania.

Wabunge hao wameeleza hayo leo Jumanne Mei 24,2026 wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa bungeni jijini Dodoma.

Mbunge wa Ikungi Magharibi mkoani Singida, Elibariki Kingu amesema Tanzania kuna wastani wa makanisa yasiyopungua 4,000 kati yao asilimia 98 ya nyumba hizo za ibada zinamilikiwa na mtu mmoja mmoja mbali na yale yanayomilikiwa na taasisi.

“Kusema Tanzania kuna ubaguzi wa kidini hapana…Wakati chini uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan tumeshuhudia kuna uhuru mkubwa wa kuabudu. Leo Rais anakwenda katika kanisa na kuendesha harambee au Muislamu anakwenda kanisa kufanya harambee,”

“Mheshimiwa Spika Taifa hili halina mambo ya kutesana kidini, ndio maana leo tunazungumza pembeni yangu ameketi mbunge Muislamu, pembeni yangu amekaa mbunge Mkristo,” amesema Kingu.

Mbunge wa Mtama mkoani Lindi, Nape Nnauye amesema Tanzania ni Taifa huru linalopaswa kuheshimiwa hata linapopitia changamoto zake za ndani.

“Tupo huru, tunathamini mchango wao, lakini muhimu wakumbuke wasitumie changamoto tulizonazo kutuumiza, kutunyanyasa na kutukandamiza,”

“Uhusiano wa Tanzania na mataifa ya nje unapaswa kuheshimu uhuru na mamlaka ya nchi na kuiitaka Serikali kuchukua hatua za kidiplomasia kumaliza mvutano huo,” amesema.

Kwa upande wake, mbunge wa Bunda Mjini, mkoa wa Mara, Esther Bulaya amesema mataifa ya Tanzania na Marekani yana uhusiano wa kihistoria hivyo suala hilo linapaswa kushughulikiwa kwa busara ili kuepusha kuharibika kwa mahusiano ya nchi hizo mbili.

Bulaya amesema Tanzania ina uhusiano mzuri wa kihistoria na Marekani na ipo tayari kuyalinda mahusiano hayo na itakuwa ya mwisho kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na nchi yoyote.

“Lakini tunatambua Taifa hili ni huru, kuna mambo ambayo sisi kama Taifa kwa sheria, kanuni na Katiba yetu tuna uwezo kushughulika nayo. Tunawaomba watu wachache wanaotaka kuvunja heshima, tamaduni mamlaka kamili ya nchi yetu, wasitumie kigezo hicho kujinufaisha kisiasa,” amesema Bulaya.