Na Mwandishi Wetu, Moscow
CHUO Kikuu mashuhuri nchini Urusi leo kimemtunukia shahada ya heshima ya Uzamivu (honoris causa) Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na uongozi usio kifani na mchango wake kwa maendeleo ya taifa lake.
Chuo hicho kinachojulikana kwa jina la Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi (RUDN) ni miongoni mwa vyuo mashuhuri duniani – kikijipatia sifa kutokana na kusomesha kada ya wasomi wa miaka ya mwanzoni ya Uhuru barani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini na kujulikana kwa jina la Patrice Lumumba.
Akipokea shahada hiyo ya heshima – ya nane tangu aingie madarakani, Rais Samia alisema amepokea tuzo hiyo kwa unyenyekevu mkubwa na haichukulii kama yake binafsi.
“Nilipopata taarifa ya kupewa hadhi hii, niliona kwamba hii heshima si yangu pekee bali ni kwa wale wote ambao elimu ina maana kwao. Kwa walimu wanaofundisha kote, kwa wanafunzi want guys maarifa na kwa wazazi wanaopambana kusomesha watoto wao.
“ Jina la chuo hiki, likichukua jina la mmoja wa viongozi wanamapinduzi wa Afrika la Patrice Lumumba ni kielelezo cha ushahidi wa uhusiano unaojali ukombozi, utu na umoja wa kweli,” alisema.
Rais Samia alitumia hotuba yake ya kupokea heshima hiyo kwa kueleza kuhusu umuhimu wa elimu akisema imebadili maisha ya watu na mataifa mbalimbali.
“Hakuna taifa linalotaka kuachwa nyuma katika dunia ya sasa yenye mabadiliko makubwa katika maeneo kama vile akili mnemba na sayansi za mashine. Jambo kubwa kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla si kwamba tuingie kwenye ushindani au la bali ni namna gani tutaingia kwenye ushirikiano na kufaidika na mabadiliko haya,” alisema.
Tukio hilo lilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Sayansi na Elimu ya Juu wa Urusi, Konstantin Mogilevsky, ambaye katika hotuba yake alisema Rais Samia ametoa mchango mkubwa katika ukuzaji wa elimu nchini kwake katika kipindi cha miaka yake sita madarakani.
RUDN imekuwa na mahusiano ya muda mrefu na Tanzania, kikiwa kimesomesha zaidi ya Watanzania 1,100 tangu kianzishwe mwaka 1960 iliyopita na sasa wanafunzi wa Kitanzania 72 wanapata mafunzo katika ngazi mbalimbali chuoni hapo.
Rais Samia anakuwa Rais wa karibuni zaidi kupewa heshima hiyo na chuo hicho, huku marais wengine sita wakiwa wamewahi kupewa tuzo hiyo. Baadhi ya marais hao ni Sam Nujoma wa Namibia, Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na Olesegun Obasanjo wa Nigeria.
Vyuo vikuu vingine saba ambavyo vimewahi kumtunukia Rais Samia shahada za namna hiyo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Jawahral Nehru nchini India, Chuo Kikuu cha Ankara nchini Uturuki, Nasarawa nchini Nigeria, Chuo Kikuu cha Anga cha Korea Kusini, Chuo Kikuu cha Mzumbe na Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).
Rais Samia yuko nchini Urusi katika ziara ya kitaifa iliyoanza jana na itahitimishwa kesho baada ya kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi wa St. Peterburg nchini hapa.
