Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Madiwani wa Manispaa ya Ubungo wamekubaliana kwa kauli moja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), wamekubaliana kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakabili wananchi na kuweka mikakati itakayosaidia kuimarisha upatikanaji huduma za Maji.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo, Mhe Lawrence Mlaki, kilitoa fursa kwa madiwani kuwasilisha changamoto za huduma ya maji katika kata zao, sambamba na kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa wananchi wa Wilaya ya Ubungo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Mlaki amesema Mkuu wa Wilaya ya Ubungo , Albert Msando ameridhishwa na hatua ya kuwakutanisha wadau mbalimbali ndani ya manispaa hiyo ili kujadili kwa pamoja changamoto za maji na kutafuta ufumbuzi wake.
“Tumepata nafasi na DAWASA ya kusikia moja kwa moja changamoto mbalimbali kutoka kwa madiwani wa kila Kata ndani ya Manispaa yetu. Tunaamini maoni na mapendekezo yaliyotolewa yatakuwa msingi mzuri wa kuboresha huduma ya maji katika maeneo yetu na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi,” amesema Mlaki.
Aidha, ameipongeza DAWASA kwa hatua zinazoendelea za ufungaji wa pampu mpya katika Mtambo wa Uzalishaji Maji wa Ruvu Juu, akisema maboresho hayo yanatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Ubungo.
“Wito wetu kwa DAWASA ni kuendelea kwa kasi na zoezi la ufungaji wa pampu mpya zitakazosaidia uhakika wa huduma, hili ni moja ya mapendekezo makubwa yaliyotolewa na Waheshimiwa Madiwani, na tunaamini litakuwa sehemu ya suluhisho la kudumu la changamoto ya maji katika wilaya yetu,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DAWASA, Mhandisi Romanus Mwangingo, amesema Mamlaka imepokea maoni, changamoto na maelekezo yote yaliyotolewa na madiwani na ipo tayari kuyafanyia kazi kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi.
“Mamlaka imejipanga kuhakikisha changamoto zote zilizowasilishwa zinapatiwa ufumbuzi huku lengo letu ni kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Ubungo wanapata huduma ya maji kwa uhakika na kwa viwango vinavyokidhi mahitaji yao,” amesema Mhandisi Mwangingo.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Mamlaka na viongozi wa wananchi katika kubaini maeneo yenye changamoto sugu za maji ili yaweze kupewa kipaumbele katika mipango ya maboresho.
