You are currently viewing Dkt Samia: Tunataka uhusiano wetu na Urusi uwe ushirikiano wa kiuchumi

Dkt Samia: Tunataka uhusiano wetu na Urusi uwe ushirikiano wa kiuchumi

Rais wa Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania inalenga kuinua na kuimarisha uhusiano wake wa muda mrefu na Urusi kwa kuupa mwelekeo mpya utakaojikita katika maendeleo ya uchumi zaidi.

Akizungumza katika mahojiano wakati wa ziara yake jijini Moscow, Rais Samia amesema ziara hiyo ni hatua muhimu ya kihistoria, akibainisha kuwa Tanzania ina dhamira ya kuonesha fursa na uwezo wake katika sekta mbalimbali muhimu zikiwemo maliasili, kilimo, afya na sayansi ya data.

Dkt Samia amefafanua kuwa Tanzania inaendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kuvutia ushirikiano mpana zaidi na uwekezaji kutoka mataifa mbalimbali.

“Tunataka kuionesha dunia Tanzania na kile tulichonacho cha kutoa, kuanzia maliasili, kilimo, fursa zilizopo katika sekta ya afya, sayansi ya data na maeneo mengine mengi yenye uwezo mkubwa wa kuchochea maendeleo,” amesema.

Aidha, Dkt Samia amesisitiza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Urusi una mizizi ya kihistoria, akisema Taifa hilo lilikuwa miongoni mwa nchi ya  kwanza kuitambua Tanzania mara baada ya kupata uhuru wake.

Ameongeza kuwa kwa kipindi cha miaka 65, nchi hizo mbili zimeendelea kudumisha uhusiano wa karibu uliojengwa zaidi katika ushirikiano wa kisiasa na mshikamano wa kidiplomasia.

Hata hivyo, amesema kwa sasa uhusiano huo unaingia katika hatua mpya ambapo Tanzania na Urusi zinakusudia kuupanua zaidi kwa kuhamia katika ushirikiano wenye msukumo mkubwa wa biashara, uwekezaji na maendeleo endelevu ya uchumi, badala ya kutegemea zaidi ushirikiano wa kisiasa na misaada kama ilivyokuwa hapo awali.