You are currently viewing Marekani yaipa Tanzania bilioni 2.6 kukabili Ebola

Marekani yaipa Tanzania bilioni 2.6 kukabili Ebola

Serikali ya Marekani imetoa zaidi ya Dola za Marekani milioni moja, sawa na takribani Sh2.63 bilioni ili kusaidia kuimarisha maandalizi na utayari wa Tanzania katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 15, 2026 na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, msaada huo umetolewa kufuatia milipuko ya hivi karibuni ya Ebola iliyoripotiwa katika Nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usalama wa afya ya Wananchi wa Tanzania.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa licha ya Tanzania kutokuwa na kisa chochote kilichothibitishwa cha Ebola hadi sasa, Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wake wa kuzuia, kugundua na kukabiliana na tishio lolote la mlipuko huo kupitia mipango ya Kitaifa ya dharura.

Kutokana na mwingiliano mkubwa wa Watu katika maeneo ya mipakani na Nchi jirani, hatua hizo zinalenga kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa macho na kujiandaa kikamilifu dhidi ya uwezekano wa kuingia kwa ugonjwa huo nchini.

Mara baada ya kutangazwa kwa milipuko ya Ebola katika ukanda huu, Wizara ya Afya iliwakutanisha Wakurugenzi wa Kiufundi, Taasisi za Serikali ya Marekani pamoja na Washiriki wengine wa kimataifa ili kuratibu maandalizi na mikakati ya kukabiliana na tishio hilo nchini kote.

Sehemu ya msaada huo itatumika kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, mifumo ya maabara, kinga na udhibiti wa maambukizi, usimamizi wa wagonjwa, mawasiliano ya hatari kwa Jamii pamoja na maandalizi katika maeneo ya kuingilia nchini.

Ubalozi wa Marekani umeeleza kuwa msaada huo utatekelezwa kupitia Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti Magonjwa (CDC), Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pamoja na Taasisi ya Utafiti ya Jeshi ya Walter Reed (WRAIR), ambayo itashirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuimarisha maandalizi katika maeneo ya mipakani yenye hatari kubwa zaidi.