Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Ubovu wa barabara kuu ya Musoma – Mwanza katika eneo la wilaya ya Magu, mkoani Mwanza umewafanya madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo kuomba Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuboresha barabara hiyo ili kupunguza ajali zinazotokea mara kwa mara na kusababisha vifo vya watembea kwa miguu pamoja na waendeshaji wa vyombo hivyo vya moto.
Pia wameshauri askari wa usalama barabarani kuongezwa katika maeneo ambayo yameharibika zaidi ili kuhakikisha madereva wanapunguza mwendo kasi katika maeneo hayo.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano na Diwani wa Kata ya Kahangara, Daud Makologoto wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, kilichopokea na kujadili taarifa mbalimbali za maendeleo kutoka kila kata, ambapo suala la ubovu wa barabara lilijitokeza kwa maeneo mengi.
“Aprili hadi Juni eneo letu limekuwa ana ajali za mara kwa mara zinazotokana na ubovu wa barabara yetu kwa kiwango kikubwa, kwenye meneo yetu tumekuwa na maumivu makubwa kwa sababu ndani ya wiki mbili nimezika wananchi wangu wawili.
“Tunaomba Serikali walichukue jambo hili kwa umuhimu kuboresha barabara yetu hususani eneo la Nyangunge – Lamadi,” amesema.
Kilio hicho cha Makologoto kiliungwa mkono na Diwani wa kata ya Nyanguge, Hilal Elisha ambaye alisema katika kuanzia Aprili hadi sasa amezika watu wanne kutokana na ajali.
Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mhandisi Edward Kihamba alikazia hoja hiyo na kumuomba mkuu wa wilaya kufikisha kilio kwa Tanroad huku akisisitiza askari wa usalama barabara kuongeza umakini katika maeneo ambayo ni mabovu zaidi.
Akizungumzia hoja hiyo kwenye kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo mbali na kueleza kusikitishwa na ajali hizo alisema ameshaagiza uongozi wa polisi wilaya hiyo kuongeza askari ili kudhibiti madereva wanaozidisha mwendokasi.
“Hakuna serikali inayopenda kupoteza wananchi wake, tumeshamuita afande OCD… ameweka polisi kwenye sehemu mbalimbali za barabara yetu katika maeneo ya Kisesa, Nyanguge na Ilungu ambapo kumekuwepo na askari wa kutosha tangu ajali zimekuwa zikiripotiwa.
“Kuna vipande vitatu au vinne vinatengenezwa hali inayosababisha wageni ambao hawaijui barabara kumiminika bila kujua hali ya barabara,” amesema.
