Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, leo tarehe 31 Julai 2026, ameongoza hafla ya makabidhiano na uzinduzi wa boti mbili za kisasa za doria, Sailfish 2 na Sailfish 3, zenye thamani ya jumla ya dola za Marekani milioni 1.6.
Boti hizo zitatumika kuimarisha ulinzi na usalama katika bahari na maziwa makuu nchini, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwekeza katika vifaa na teknolojia za kisasa zitakazoongeza uwezo wa taasisi husika kukabiliana na uhalifu na kulinda mipaka pamoja na rasilimali za Taifa kupitia maji.
Kila boti ina injini tatu zenye nguvu ya Horse Power (HP) 900, uwezo wa kwenda kwa kasi ya hadi noti 52, sawa na kilomita 96.3 kwa saa, urefu wa mita 12 na uwezo wa kubeba watu 12 kwa wakati mmoja.
Aidha, boti hizo zimefungwa mifumo ya kisasa ya urambazaji pamoja na vifaa vya usalama na uokoaji, vitakavyowezesha utekelezaji wa operesheni kwa ufanisi katika mazingira mbalimbali ya bahari na maziwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Dkt. Nchemba amezitaka Wizara na taasisi zinazohusika kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya uendeshaji na matengenezo ya boti hizo ili ziendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kudumu kwa muda mrefu.
Pia, amesisitiza kila Wizara na taasisi kusimamia kikamilifu majukumu yake na kuimarisha ushirikiano kati ya pande zote mbili za Muungano ili kuziba mianya inayoweza kutumiwa na wahalifu katika maeneo ya bahari na maziwa makuu.
Waziri Mkuu amezitaka taasisi zote zinazotekeleza majukumu kupitia Kituo cha Kitaifa cha Pamoja cha Operesheni kuhakikisha zinapeleka wawakilishi wanaohitajika ili kuimarisha uratibu na utekelezaji wa operesheni za pamoja.
Ameeleza kuwa ushirikiano, uratibu madhubuti na matumizi sahihi ya teknolojia ya kisasa ni msingi wa kuimarisha usalama wa mipaka ya majini na kuweka mazingira salama yatakayochochea ukuaji endelevu wa uchumi wa buluu.
