Rais Samia Suluhu Hassan, amewaalika wageni kutoka mataifa mbalimbali kutembelea Tanzania ili kujionea utajiri wa vivutio vya utalii, urithi wa utamaduni pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini.
Akizungumza leo Agosti 5, 2026 katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu kwa Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Samia amesema Tanzania ina nafasi kubwa katika sekta ya utalii na uwekezaji kutokana na rasilimali zake za asili, mazingira rafiki ya biashara na utamaduni wake wa kipekee.
“Ninawaalika mje muione Tanzania. Mjionee ukarimu wa watu wetu, utajiri wa utamaduni wetu na uzuri wa nchi yetu. Kuanzia tambarare za Serengeti, Mlima Kilimanjaro hadi visiwa vya kuvutia vya Zanzibar, Tanzania inatoa uzoefu wa kipekee wa utalii na fursa nyingi za uwekezaji,” amesema Rais Samia.
Amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kuweka mikakati itakayowezesha kuvutia wawekezaji zaidi, kukuza uchumi na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama eneo lenye fursa mbalimbali za maendeleo.
Aidha Rais Samia amesisitiza kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na wawekezaji na wadau wa kimataifa kutumia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali kwa ajili ya kukuza uchumi na kuleta manufaa kwa wananchi.
