Siku chache kabla ya kuanza kwa Tamasha la Kizimkazi litakalofanyika Agosti 12 hadi 14 mwaka huu, wakazi wa Kizimkazi wamesema maandalizi yamekamilika kwa ajili ya kuwapokea wageni wanaotarajiwa kushiriki tukio hilo linalolenga kukuza utalii, biashara na uchumi wa buluu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema wamejipanga kuhakikisha wageni wanapata huduma bora, mazingira salama na mapokezi mazuri yatakayowawezesha kufurahia tamasha hilo kwa utulivu.

Mkazi wa Kizimkazi Mkunguni, Thabit Khamis Majisu, amesema jamii imejipanga kuhakikisha wageni wote wanapata huduma bora na uzoefu mzuri utakaoifanya Kizimkazi kuendelea kujulikana zaidi ndani na nje ya Zanzibar.
Kwa upande wake Mkazi wa Mkunguni, Lila Mikidadi Mwinyi, amesema wakazi wa Kizimkazi wameungana kufanya usafi katika mitaa na maeneo ya umma ili kuonyesha utayari wao wa kuwapokea wageni, hatua inayolenga kuimarisha taswira ya Kizimkazi kama kitovu cha utalii, biashara na uwekezaji.
Tamasha hilo lenye kaulimbiu “Kizimkazi Kumenoga: Shangwe na Fursa” linatarajiwa kufungua fursa za uwekezaji, kukuza utalii, biashara na maendeleo ya jamii.
