Rais Samia Suluhu Hassan leo Agosti 7, 2026 amezindua Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Wahusika wa Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria katika Matukio ya Ghasia Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, yenye Makamishna sita, wakiwamo majaji wawili kutoka nje ya nchi.
Uzinduzi huo umefanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, ukifuatia uteuzi wa wajumbe wa tume hiyo uliofanywa Mei 18, 2026. Kuundwa kwa tume hiyo kunatekeleza moja ya mapendekezo ya Tume ya Kuchunguza Matukio ya Vurugu Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman.
Tume hiyo inaongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Shabani Lila, ambaye ni Mwenyekiti na Kamishna. Makamishna wengine kutoka Tanzania ni Jaji Mstaafu Gad Mjemmas, Jaji Mstaafu Awadh Bawazir na Jaji Mstaafu Aishieli Sumari, wote wakiwa ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu.
Makamishna kutoka nje ya nchi ni Petrus Tileinge Damaseb wa Namibia na Cheborion Barishaki kutoka Uganda.
Damaseb anahudumu kama Naibu Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Namibia na pia ni Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Namibia, huku Barishaki akiwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Uganda, ambayo pia hufanya kazi kama Mahakama ya Kikatiba ya Uganda, pamoja na kuwa Jaji wa Kitengo cha Rufani cha Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki.
