You are currently viewing DC Magu azindua kongamano la vijana, wapewa mbinu kujikwamua kiuchumi

DC Magu azindua kongamano la vijana, wapewa mbinu kujikwamua kiuchumi

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

MKUU wa Wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo leo Jumapili amefungua kongamano la vijana kuelekea mapokezi ya Mwenge wa Uhuru na kuwataka vijana hao kuwa wazalendo na kufuata maadili ya kitanzania.

Pia vijana hao wametakiwa kutumia mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kuwa wabunifu na kujikwamua kiuchumi.

Dk. Francis Daudi akizungumza na vijana waliohudhuria kongamano hilo mjini Magu

Akifungua kongamano hilo wilayani Magu, mkoani Mwanza, Lawuo amewaasa vijana hayo kutofuata mkumbo kwa kutumia mabadiliko hayo ya teknolojia kwa kulitumbukiza Taifa shimoni.

“Natamani tukawe mabalozi wa kuongea na vijana wenzetu kwamba wasiwe watu wa kufuata mkumbo. Ninawasihi tuwe wazalendo, tusikilize kinachotolewa leo na wakufunzi wetu lakini pia tufuate uadilifu wa mtanzania,” amesema.

Kwa upande wa Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Said Zuberi amesema vijana wana nafasi kubwa ya kujenga taifa hasa ikizingatiwa asilimia 75 ya nguvu kazi ni vijana.

“Lakini pia vijana ni asilimia 35 ya watanzania hivyo, tunawategemea ninyi. Nawasihi kutumia fursa ya mabadiliko ya teknolojia kwa umakini na kutambua fursa mbalimbali zilizopo kwa maendeleo ya vijana,” amesema.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Mohamed Ramadhani aliwasihi vijana hao kuendelea kuchangamkia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri hiyo lakini pia kuwa waaminifu na kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.

“Licha ya kuwepo kwa fursa ya vijana kukopeshwa, bado vijana tumeendelea kupoteza uaminifu wa kutumiwa na hata na watu kwenye  biashara zao. Ninawasihi kijana zinduka, jiweke sawa kutumia fursa hizi,: amesema.

Aidha, akitoa mada katika kongamano hilo, Mkufunzi kutoka Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dk. Francis Daud aliwasisitiza vijana hao kujijenge tabia ya kuweka akiba pamoja na kuwekeza katika mifuko mbalimbali nchini ili kujikwamua kiuchumi.

Awali akifungua kongamano hilo, Afisa Vijana wilaya ya Magu Prisca Salum alisema kongamano hilo linalenga kuhamasiaha vijana kujipanga kuupokea mwenge wa uhuru katika wilaya hiyo tarehe 12 Agosti mwaka huu.

Baadhi ya vijana walioshiriki kongamano hilo, akiwamo Baraka Ramadhani na Bwisu Weja mbali na kuushukuru uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Magu kwa kuandaa kongamano hilo, pia walisema mafunzo waliyoyapata yamewafungua macho na kutambua fursa mbalimbali muhimu za kujikwamua kiuchumi.