You are currently viewing RC Chalamila aagiza TANROADS kudhibiti maegesho holela, malori 50 yakamatwa
Malori yakiwa yameegeshwa kiholela

RC Chalamila aagiza TANROADS kudhibiti maegesho holela, malori 50 yakamatwa

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameagiza kuchukuliwa kwa hatua kali dhidi ya madereva wa malori wanaopaki kwenye hifadhi ya barabara (service roads) na kusababisha kuzibwa kwa njia pamoja na kuongezeka kwa msongamano wa magari jijini.

Akizungumza leo Jumatatu Agosti 17, 2026 katika Barabara ya Mandela, Wilaya ya Temeke, wakati wa ziara ya kukagua mwenendo wa utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa hivi karibuni,  Chalamila amesema Mkoa wa Dar es Salaam hautavumilia tena vitendo vya uholela vinavyohatarisha usalama na kuvuruga matumizi sahihi ya miundombinu ya barabara.

Amesisitiza kuwa mamlaka zinapaswa kusimamia sheria kwa msimamo bila mizaha wala unafiki, akieleza kuwa wakati umefika wa kurejesha hadhi na heshima ya Jiji la Dar es Salaam.

RC Chalamila ameiagiza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuweka vizuizi katika maeneo ya service roads ili kuzuia malori kuingia na kuyatumia kama maeneo ya maegesho.

Aidha, ameiagiza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na maafisa wa Mkoa kuwakamata madereva watakaokaidi maagizo hayo.

Pia amezitaka Halmashauri na wakuu wa Polisi wa Wilaya kuweka vikosi maalumu vya kusimamia barabara na kuhakikisha njia zinapitika bila msongamano unaosababishwa na maegesho yasiyo rasmi.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, amesema wameanza kutekeleza maagizo hayo mara moja, huku operesheni ikipita maeneo ya Shekilango, Ubungo, Tabata, Tazara na Kurasini.

Kyamba amesema TANROADS inatumia magari ya breakdown kuondoa malori yaliyopaki kwenye service roads na kuyapeleka ofisini, huku wahusika wakitakiwa kulipa faini pamoja na gharama za kuvutwa kwa magari yao.

Amesema zaidi ya malori 50 yalikuwa tayari yamekamatwa na kufikishwa ofisini wakati operesheni hiyo ikiendelea. Amesisitiza kuwa service roads zimejengwa kwa ajili ya dharura na kuruhusu magari yanayotoka majumbani kuingia kwenye barabara kuu, si kwa ajili ya maegesho ya malori