Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimempendekeza Deogratius John Ndejembi kuwa Makamu mpya wa Rais wa Tanzania, baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Dk. Emmanuel Nchimbi, kujiuzulu.
Uamuzi huo umefikiwa na Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.
Iwapo atathibitishwa kwa mujibu wa taratibu za kikatiba, Ndejembi mwenye umri wa miaka 43 atachukua nafasi iliyoachwa na Nchimbi, ambaye alijiuzulu baada ya kuitumikia kwa takriban miezi 10.
Na akithibitishwa pia Ndejembi atakuwa Makamu wa rais wa 13 tangu Tanzania ipate uhuru, akiwa miongoni mwa Makamu wa raisi vijana zaidi kuwahi kushika nafasi hiyo.
Ndejembi, ambaye amekuwa Waziri wa Nishati tangu mwaka 2025, anaingia katika kinyang’anyiro hicho akiwa na uzoefu wa zaidi ya muongo mmoja katika siasa na utumishi wa umma, lakini safari yake haikuanza serikalini.
Kabla ya kuingia kwenye uongozi wa serikali, Ndejembi alifanya kazi katika sekta binafsi. Mwaka 2012 alikuwa meneja wa kampuni ya A1 Outdoor, kabla ya kuwa Mkuu wa Mauzo katika kampuni ya Smile Communication kati ya mwaka 2012 na 2014.
Mwaka 2014 alijiunga na Tigo kama Meneja wa Kanda, nafasi aliyoshikilia hadi mwaka 2015, na mwaka 2016 alikuwa Mkuu wa Masoko wa GSM Group.
