Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, amesema kupata uzoefu na kuondoa dhana ya watendaji kujenga ‘falme’ katika maeneo wanayohudumu ni miongoni mwa sababu zilizomfanya kufanya mabadiliko na kuwahamisha baadhi ya wakuu wa mikoa.
Dkt Samia ameeleza hayo Jumatano Septemba 2,2026 wakati wa akiwaapisha wakuu wa mikoa na katibu tawala aliowateua hivi karibuni. Uapisho huo umefanyika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Kusini Unguja.
“Moja ni kupata uzoefu kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine. La pili, kutotengeneza ufalme pale ulipo, kwamba ndio kwangu na himaya ulizozijenga ndio za kwako. Hapana, wewe ni mtumishi wa umma, unaweza kutumika popote pale,” ameeleza.
Rais Samia amekumbusha kuwa katika mkutano wake wa mwisho na wakuu wa mikoa aliwaambia kuwa yeye anawachukulia kama jeshi lake, hivyo hatarajii kuona jeshi hilo likichafuka.
“Huko mliko nimekuwa nikipata taarifa hizi, zile; huyu ana hivi, huyu ana lile. Sasa kuwabadilisha ni kuwaondosha katika matatizo yale ambayo nayapokea. Sasa kama ulikuwa unajijua una tabia mbaya au yoyote, nenda kajirekebishe, tumikia wananchi kama inavyotakiwa,” amesema Dkt Samia.
