You are currently viewing CMT – Magu yakagua miradi ya maendeleo, yaagiza hadhari dhidi ya el nino

CMT – Magu yakagua miradi ya maendeleo, yaagiza hadhari dhidi ya el nino

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhan ameongoza Timu ya Menejimenti ya Halmashauri (CMT) kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata za Kisesa, Bujora na Bukandwe kwa lengo la kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora, kwa wakati na kwa thamani halisi ya fedha.

Pia imekagua na kutoa ushauri kuhusu miundombinu ya mitaro iliyopo katika eneo la Stendi ya Kayenze ili kujihadhari na ujio wa mvua kubwa za El nino zinazotarajiwa kuanza mwezi Oktoba mwaka huu.

Katika ukaguzi huo uliofanyika jana Jumatatu, Mkurugenzi huyo pia alizingumza na wananchi na kuwaomba kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi hiyo kwani inalenga kuboresha sekta mbalimbali wilayani humo.

Miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule mpya ya Msingi Igewe iliyopo Kijiji cha Wita kata ya Kisesa.

Maboresho ya Stendi ya Kayenze iliyopo kata ya Bukandwe kwa lengo la kukabiliana na ujio wa mvua za El nino pamoja na ukaguzi wa eneo la ujenzi wa fremu za biashara katika uwanja wa Ngomeni uliopo kata ya Bujora.

Akizungumza na wananchi katika eneo la ujenzi wa shule hiyo ya msingi Igewe, DED Ramadhani aliwapongeza wananchi hao kwa jitihada walizozionesha katika kuanzisha ujenzi huo, lakini pia aliwasisitiza kuendelea kutoa ushirikiano katika kukamilisha mradi huo pamoja na kulinda mipaka ya eneo la shule hiyo.

Aidha, Timu ya Menejimenti ya Halmashauri (CMT) ilihimiza usimamizi wa karibu wa miradi, utunzaji wa nyaraka na uwajibikaji katika kila hatua ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Miradi hii inalenga kuboresha huduma za elimu kwa watoto, kuongeza fursa za ajira na kipato kwa wananchi na mapato kwa halmashauri, kuimarisha miundombinu na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu.