Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhani amewaagiza watendaji wa kata pamoja na maofisa afya wa wilaya hiyo kuendelea kuelimisha jamii namna ya kujikinga na maafa yanayoweza kutokea kutokana na mvua kubwa za El nino zinazotarajiwa kuanza Oktoba hadi Disemba mwaka huu.
Pia amewaagiza kuboresha mawasiliano pamoja na kubainisha maeneo ambayo ni hatarishi kutokana na mafuriko hayo pamoja na kuchukua hatua za haraka ili kupunguza athari za mvua hizo iwapo kukitokea maafa.
Mkurugenzi huyo ametoa maagizo hayo jana Septemba 16 mwaka 2026 alipozungumza na watendaji hao kwa lengo la kuwaelekeza namna ya kutekeleza mpango kazi wa halmashauri katika kukabiliana na mvua hizo za El nino.
Amewataka maofisa afya kuhakikisha wananchi wote ndani ya halmashauri wanashiriki kikamilifu katika zoezi la usafi wa mazingira katika maeneo yao pamoja na kuzibua mitaro iliyozibwa kutokana na utupaji taka ovyo.
“Tuhakikishe wanatupa taka katika maeneo maalum yaliyotengwa. Waache kuchafua barabara, mitaro, masoko na maeneo ya wazi. Tuwasimamie wasafishe maeneo yanayozunguka nyumba, biashara na maeneo ya kazi.
“Lakini pia watunze mifereji na mitaro ili kuzuia kuziba na kusababisha mafuriko. Tuhakikishe wamejenga na kutumia vyoo safi. Wale wenye tabia ya kutotiririsha majitaka ovyo waonywe na kuchukuliwa hatua,” alisema.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Magu, Dk. Raphael Mhana alisema hospitali ya wilaya, vituo vya afya pamoja na zahanati zote tayari zimejiandaa iwapo kutatokea maafa yoyote.
“Vifaa tiba vinavyotakikana vipo vya kutosha, vimesambazwa kwenye kila kituo ili kuhakikisha magonjwa ya mlipoko kama kipindupindu hayaleti madhara wala kuathiri wilaya yetu. Lakini pia elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi ili kujikinga na magonjwa haya,” alisema.
Aidha, Mtendaji wa kata ya Nyangunge, Wilybroad Mbuga alisema watatumia mikunyiko mbalimbali kama vile kwenye makanisa, misikiti, sherehe, misiba kuwaelimisha wananchi kuhusu athari za mvua za El nino kuwaeleza athari inayoweza kutokea.
