WANANCHI wa kata ya Ng’haya na kata jirani za wilaya ya Magu mkoani Mwanza wameeleza kunufaika na ujenzi wa daraja la Sukuma ambalo ujenzi wake sasa umefikia asilimia 86.
Daraja hilo linalotarajiwa kukamilika Disemba mwaka huu, limetengeneza ajira zaidi 71, huku wajasiriamali wadogo ikiwamo wa huduma ya chakula, wakieleza kunufaika na ujenzi wa daraja hilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi hao, akiwamo Rehema Sylivesta ambaye ni mkazi wa Ng’hanya, amesema kwa upande wake ameajiriwa kuwa mtoa huduma katika eneo hilo jambo ambalo limemsaidia kupata kipato kwa kipindi hiki cha ujenzi.
Naye Nkwabi Wilson ambaye pia ni mkazi wa Ng’haya ameishukuru serikali kwa ujenzi wa daraja hilo hasa ikizingatiwa kukamilika kwake kutawasaidia kurahisisha shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
“Tutafurahi kuisha kwa mradi huu kwa sababu tutakuwa na uhakika wa kufanya shughuli zetu za kiuchumi ikiwamo usafirisha wa mazao hasa ikizingatiwa daraja hili linaunganisha wilaya ya Magu na Bariadi,” alisema.
Awali Msimamizi miradi ya maendeleo kutoka Wakala wa barabara mkoa wa Mwanza (Tanroad), Mhandisi Wiliam Sanga amesema ujenzi wa daraja hilo umewanufaisha wananchi kwa namba mbalimbali kwani jumla ya wananchi 53 walilipwa fidia ya Sh milioni 127 ili kuwezesha ujenzi wa barabara za maingilio kwa upande wa Lumeji na Busaranga.
Daraja hilo linajengwa na kampuni ya Mkandarasi Mzawa ya Mumangi Construction Ltd.
