You are currently viewing TPA kuboresha huduma kwa wateja kukabiliana na ushindani soko  kimataifa

TPA kuboresha huduma kwa wateja kukabiliana na ushindani soko  kimataifa

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeweka mkazo katika kuongeza ufanisi wa huduma na kupanua miundombinu ya bandari zake ili kukabiliana na ongezeko la meli na mizigo, huku ikiimarisha ushindani wa bandari nchini katika soko la kimataifa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja yenye kaulimbiu “Hatua ya Ziada”, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, Balozi Ernest Mangu, alisema mafanikio yanayoendelea kupatikana katika bandari yameongeza mzigo wa kazi, hivyo watendaji wanapaswa kuongeza ufanisi ili kuendelea kuimarisha imani ya watumiaji wa huduma hizo.

Balozi Mangu ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi ( IGP) mstaafu alisema ongezeko la mizigo limeibua changamoto nyingine, ikiwamo msongamano wa malori katika barabara zinazoelekea bandarini na katika vituo maalumu vya kuhifadhi na kushughulikia mizigo (ICDs).

Hivyo, aliwataka TPA, wasafirishaji na wadau wengine wa sekta ya usafirishaji na usafirishaji wa mizigo kushirikiana kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo ili kuhakikisha ukuaji wa shughuli za bandari hauathiri ufanisi wa huduma.

Alisema TPA inapaswa kutumia ubunifu na kubaini mapungufu ya kiutendaji ndani ya taasisi hiyo badala ya kutegemea zaidi kutafuta wateja wapya, akisisitiza kuwa ufanisi wa huduma ndiyo msingi wa kuvutia na kuwahifadhi wateja katika soko lenye ushindani mkubwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es salaam Bw. Abed Gallus (katikati) kwa kushirikiana na wadau wa (TPA) kutoka katika Makampuni tofauti tofauti wakishiriki katika zoezi la ukataji wa keki uliofanyika wakati wa hafla ya uzinduzi wa wiki ya huduma kwa mteja iliyofanyika katika ofisi za makao makuu Dar es salaam.

“Lengo letu ni kuhakikisha bandari zinaendelea kuwa kiungo muhimu katika kukuza uchumi na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Sekta ya umma inahitaji kushirikiana na sekta binafsi katika kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050,” alisema.

Katika hafla hiyo, Balozi Mangu pia alitoa tuzo kwa wafanyakazi 12 waliofanya vizuri kutoka idara mbalimbali za TPA, huku akiwataka kuendelea kuongeza bidii na ubunifu ili kudumisha kiwango cha utendaji na kuwa mfano kwa watumishi wengine.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, alisema Wiki ya Huduma kwa Wateja in lengo la kuhimiza watendaji kwenda hatua ya ziada katika kuhakikisha wateja wanapata huduma bora wakati wote.

“Pamoja na maendeleo makubwa yaliyofanyika hapa bandarini, tunaishukuru Serikali kwa kuturuhusu kukopa fedha kwa ajili ya kuendelea kuboresha bandari zetu kiasi cha dola milioni 500 za Marekani,” alisema Mbossa.

Alisema miongoni mwa miradi inayotekelezwa ni ujenzi wa matanki 15 ya kupokelea na kuhifadhi mafuta katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam, wenye thamani ya Sh bilioni 678.641, ambao umefikia asilimia 52 ya utekelezaji.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania Balozi Ernest Mangu akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa TPA waliotunukiwa tuzo ya kufanya kazi bora kwa kutoa huduma kwa wateja, tukio hili limefanyika katika siku ya uzinduzi wa wiki ya huduma kwa mteja iliyofanyika katika ofisi za makao makuu Dar es salaam, kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Plasduce Mkeli Mbossa na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es salaam Bw. Abed Gallus.

Aidha, alisema TPA inaendelea kuboresha Kituo cha Kilojistiki cha Kurasini chenye ukubwa wa mita za mraba 80,000, kitakachotumika kupokea na kuhifadhi makasha, maegesho ya magari pamoja na kuboresha barabara na mifumo ya umeme, ulinzi na huduma nyingine muhimu.

“Pamoja na maboresho hayo, tunafanya pia ujenzi wa Gati la Malindi lililopo hapa Dar es Salaam, mbele ya Makao Makuu ya Mamlaka,” alisema Mbossa.

Alisema mradi huo unahusisha uboreshaji wa eneo la takribani mita 500 pamoja na uchimbaji wa kina cha bahari ili kurahisisha meli kufika katika gati hilo, huku utekelezaji wake ukiwa umefikia asilimia 15.

Mbossa alisema maboresho mengine yanafanyika katika Bandari ya Mtwara, yakilenga kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena zinazoweza kuchafua mazingira, zikiwamo makaa ya mawe, saruji na bidhaa nyingine zinazofanana, ambapo utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 49.

Alisema TPA pia inaendelea na ujenzi wa Bandari ya Kisasa ya Mbambabay iliyopo katika Ziwa Nyasa, ambao umefikia asilimia 60, pamoja na ujenzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini ambao umefikia asilimia 78.

Aidha, alisema Mamlaka ina mpango wa kuboresha zaidi Bandari ya Dar es Salaam kwa kujenga Gati Namba 12 hadi 15 na kuimarisha Gati Namba 8 hadi 11, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia meli na mizigo kwa ufanisi zaidi.