You are currently viewing Spika Bunge la Uingereza aipongeza Tanzania kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi

Spika Bunge la Uingereza aipongeza Tanzania kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi

Spika wa Bunge la Uingereza, Sir Lindsay Hoyle, amesema Tanzania ni mshirika muhimu katika kukuza uchumi na biashara, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya Tanzania na Uingereza.

Akizungumza katika mahojiano yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) jijini Arusha, Sir Lindsay amesema kuimarisha uhusiano huo kutasaidia kufungua fursa mpya kwa nchi hizo mbili na kujenga zaidi juu ya uhusiano wao wa kihistoria.

Ameitaja Tanzania kuwa injini muhimu ya uchumi wa Afrika Mashariki, kutokana na fursa zinazotokana na idadi kubwa ya vijana wenye elimu, utalii, rasilimali za gesi asilia na kuongezeka kwa uwezo wa uzalishaji wa umeme.

Sir Lindsay pia amepongeza uongozi wa Tanzania na nafasi yake inayokua katika kukuza diplomasia ya kibunge, maendeleo ya kiuchumi na ushirikiano wa kimataifa, akieleza kuwa Tanzania ina nafasi muhimu katika kukuza ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

“Kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya Tanzania na Uingereza kutakuwa muhimu katika kufungua fursa na kutumia ipasavyo uwezo wa nchi zote mbili, sambamba na kujenga juu ya uhusiano wetu wa kihistoria,” amesema Sir Lindsay

Katika eneo la usawa wa kijinsia, Spika huyo ameipongeza Tanzania kwa hatua ilizopiga katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika kufanya maamuzi ya kisiasa.

Amesema Tanzania kuwa na Rais wake wa kwanza mwanamke pamoja na wanawake kuwa na uwakilishi wa asilimia 39.5 Bungeni ni ishara ya hatua kuelekea usawa zaidi wa kijinsia.

#IPU153Tanzania