You are currently viewing Washiriki IPU 153 wajionea fursa zilizopo Tanzania

Washiriki IPU 153 wajionea fursa zilizopo Tanzania

Wajumbe na wahudhuriaji wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), wameendelea kutembelea Banda la Karibu Tanzania, linalotoa fursa kwa wageni kujionea utamaduni, vivutio na mafanikio mbalimbali ya Tanzania, pamoja na kupata taarifa kuhusu fursa za uwekezaji na maendeleo nchini.

Banda hilo limekuwa miongoni mwa vivutio katika mkutano huo unaofanyika jijini Arusha na kuwashirikisha zaidi ya wajumbe 2,000 kutoka mataifa 184 duniani.

Wageni wanaotembelea banda hilo wanapata fursa ya kujionea na kupewa maelezo kuhusu miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa nchini, ikiwamo Reli ya Kisasa ya (SGR), Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), Bandari ya Dar es Salaam na miundombinu inayohusiana na maandalizi ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Aidha, wageni wanaelezwa kuhusu Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 na hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), huku wakipata fursa ya kufahamu maendeleo yanayofanyika katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

#IPU153Tanzania