You are currently viewing Kihongosi ambana mkandarasi wa daraja la Mohoro, ataka likamilike kwa wakati 

Kihongosi ambana mkandarasi wa daraja la Mohoro, ataka likamilike kwa wakati 

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, amemtaka mkandarasi anayejenga Daraja la Mohoro wilayani Rufiji, mkoani Pwani, kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili kuwaondolea wananchi adha ya mafuriko.

Daraja hilo linajengwa kwa gharama ya Sh bilioni 17.8, huku zaidi ya Sh bilioni tisa zikiwa tayari zimetolewa na utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 72.

Kihongosi ametoa agizo hilo leo wakati wa siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili mkoani Pwani, baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo.

Amesema kukamilika kwa daraja hilo kutasaidia kuzuia madhara yanayosababishwa na mafuriko, ambayo kwa miaka iliyopita yalisababisha maafa makubwa kutokana na daraja la awali kushindwa kumudu wingi wa maji.

“Eneo hili limegharimu maisha ya watu wengi kutokana na mafuriko. Miaka kadhaa iliyopita, maafa makubwa yalitokea hapa kwa sababu daraja lililokuwapo awali halikuweza kumudu wingi wa maji,” amesema Kihongosi.

Ameongeza kuwa baada ya changamoto hizo, serikali ilitafuta fedha kwa ajili ya kujenga daraja jipya, hatua inayowezesha wananchi kushuhudia utekelezaji wa mradi huo wenye manufaa kwao.

Hata hivyo, Kihongosi amesema ziara yake inalenga kufuatilia utekelezaji wa ahadi zilizotolewa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kujiridhisha na kiwango cha utekelezaji wake.

Vile vile, amesema mkataba wa awali ulipanga mradi huo kukamilika mwaka 2024, lakini changamoto mbalimbali zilisababisha kuchelewa kwake, huku akieleza kuwa sasa unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.

“Mnaosimamia ujenzi huu mnapaswa kutambua kuwa wananchi wanahitaji daraja hili likamilike na lianze kutumika. TARURA na mkandarasi tunahitaji mradi ukamilike kwa wakati,” amesisitiza.

Pia, amewataka wananchi wa Mohoro kutunza miundombinu hiyo ili iendelee kuwanufaisha wao na vizazi vijavyo.

Kadhalika, amesema daraja hilo ni miongoni mwa miradi muhimu ya miundombinu inayolenga kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo, akihusisha utekelezaji wake na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwaletea maendeleo wananchi wa Rufiji.