You are currently viewing Mshindi wa Miss Grand International 2026, apokewa kwa shangwe Tz

Mshindi wa Miss Grand International 2026, apokewa kwa shangwe Tz

Mshindi wa taji la Miss Grand International 2026, Jihan Dimack, amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, akirejea kutoka Thailand.

Jihan amepokelewa kwa shangwe na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania, waliokusanyika kumpongeza kwa kuiwakilisha vyema nchi hiyo katika jukwaa la kimataifa la urembo.

Mapokezi hayo yamehudhuriwa na wasanii, akiwemo Rayvanny, pamoja na wadau mbalimbali wa tasnia ya urembo na burudani nchini Tanzania.

Akiwa nchini Thailand kwa ajili ya kushiriki shindano hilo, Jihan alitoa wito kwa mataifa duniani kuendeleza amani, upendo na umoja. Alieleza kuwa watu wengi wasio na hatia wanaendelea kupoteza maisha, familia zao, makazi na ndoto zao kutokana na migogoro inayoendelea katika maeneo mbalimbali duniani.

Jihan amesema anajivunia kuzaliwa Tanzania, nchi anayoitaja kuwa mfano wa amani, upendo na umoja. Alieleza kuwa Watanzania wana utamaduni wa kuishi na kufanya kazi kwa ushirikiano, bila kujali tofauti za asili, dini au mila.

Alisisitiza kuwa amani ni ishara ya ujasiri, wala si udhaifu.

“Haijalishi unatoka wapi, tuuache ubinadamu upewe nafasi yake na tusiruhusu mioyo yetu kutawaliwa na chuki. Tueneze amani na upendo, na tuishi kwa maelewano. Asanteni,” amesema Jihan.