You are currently viewing Maajabu ya Saanane: Utalii wa gharama nafuu katikati ya jiji la Mwanza

Maajabu ya Saanane: Utalii wa gharama nafuu katikati ya jiji la Mwanza

Ungependa kujionea simba, pundamilia na swala bila kusafiri safari ndefu au kutumia gharama kubwa? Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane jijini Mwanza inakupa fursa hiyo ya kipekee! Ikiwa dakika tano tu kwa boti kutoka Capri Point, hifadhi hii inathibitisha kuwa kufurahia utalii wa asili si lazima kuwe ghali. Kwa shilingi 14,000 tu kwa mtu mmoja, unapata kifurushi kinachojumuisha usafiri wa boti, kiingilio cha hifadhi na huduma ya mwongoza wageni.

Ukaribu wake na katikati ya jiji unaifanya Saanane kuwa chaguo bora kwa mapumziko ya wikendi, matembezi ya kifamilia au ziara na marafiki. Huhitaji kukodi gari la gharama kubwa wala kupanga safari ndefu; unachohitaji ni muda kidogo wa kujitenga na pilikapilika za kila siku na kujipa nafasi ya kufurahia maajabu ya mazingira ya asili.

Ukifika kisiwani, utapokelewa na upepo mwanana wa Ziwa Victoria, mandhari ya kuvutia na fursa ya kuwaona wanyamapori kama simba, pundamilia na swala katika mazingira yao ya hifadhi. Pia, miamba mikubwa ya kuvutia inakupa fursa ya kupiga picha za kumbukumbu, huku maeneo ya kupumzika yakikupa nafasi ya kufurahia muda bora na familia au marafiki.

Zaidi ya mandhari na wanyamapori, ziara yako inaongozwa na askari na waelekezaji wa hifadhi kwa kuzingatia taratibu za usalama. Kwa hiyo, usisubiri likizo ndefu wala kuwa na bajeti kubwa ndipo ufurahie utalii. Chagua Kisiwa cha Saanane, jijengee kumbukumbu zisizosahaulika na ugundue kuwa maajabu ya utalii yako karibu nawe kuliko unavyofikiri. 

Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane inatoa huduma ya kipekee ya kukodisha viwanja vya wazi kando ya Ziwa Victoria kwa ajili ya harusi, sherehe za kuzaliwa, na matukio ya makampuni kuanzia asubuhi hadi mapema jioni.

Malazi katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane yanajumuisha kambi ya umma (Public Campsite) iliyopo umbali wa mita 500 kutoka geti kuu. Katika eneo hili, wageni wana fursa ya kuleta na kupiga mahema yao binafsi au kukodisha mahema ya kisasa yenye matandiko yanayotolewa na uongozi wa hifadhi kwa ajili ya usalama na faraja yao.

Mahema haya yanaruhusu wageni kulala ndani ya kisiwa huku wakifurahia vitanda vya kisasa, bafu za ndani, na mtazamo wa kipekee wa mawimbi na upepo mwanana kutoka Ziwa Viktoria wakati wa usiku.

Kisiwa hiki kinatoa fursa nzuri za burudani na michezo ya nje kwenye mandhari yake ya kuvutia. Wageni wanaweza kufurahia shughuli kama vile kutembea kwa miguu (hiking) kwenye miamba mikubwa ya granite, kuvua samaki kwa burudani (sport fishing), kupiga picha za machweo, pamoja na kupumzika kwenye maeneo maalum ya picnic yaliyotandazwa kote kisiwani.