You are currently viewing Magereza: Lissu hajagoma kula, mawakili hawajazuiwa kumtembelea

Magereza: Lissu hajagoma kula, mawakili hawajazuiwa kumtembelea

JESHI la Magereza limesema Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, hajagoma kula chakula na kwamba mawakili wake watatu hawajazuiwa kumtembelea gerezani, likisisitiza kuwa wanaruhusiwa kumuona kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Oktoba 27, 2026, Msemaji wa Jeshi la Magereza, Elizabeth Mbezi, amesema Lissu yupo salama na amekanusha taarifa zilizodai kuwa ameingia katika mgomo wa kula.

“Jeshi la Magereza linapenda kuujulisha umma kwamba mahabusu Tundu Lissu yupo salama na hayupo katika mgomo wa kula chakula kama ilivyoripotiwa,” amesema Mbezi.

Kuhusu madai ya kuzuiwa kwa mawakili wa Lissu kuonana naye, Mbezi amesema wameendelea kuruhusiwa kumtembelea mteja wao baada ya kuthibitisha kuwa ni mawakili wake na kwa kuzingatia taratibu za gereza.

Aidha, Jeshi la Magereza limewataka Watanzania kupuuza taarifa linazodai kuwa zinapotosha kuhusu hali ya Lissu, likieleza kuwa zinaweza kuleta taharuki katika jamii.