You are currently viewing Tume yaanza kuwabaini waliopanga na kufadhili ghasia za uchaguzi 2025

Tume yaanza kuwabaini waliopanga na kufadhili ghasia za uchaguzi 2025

Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 imesema imeanza uchunguzi watu waliopanga, kufadhili, kuratibu na kushiriki katika ghasia zilizotokea kipindi hicho.

Hatua hiyo imekuja baada ya Tume hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti Jaji Shabaan Lila kuwaambia waandishi wa habari kuwa Tume imeshakamilisha uchunguzi wa awali kuhusu matumizi ya nguvu katika kudhibiti vurugu hizo.

Kwa mujibu wa Jaji Lila,  Tume imekamilisha ukusanyaji wa ushahidi katika wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam na sasa inaanza kutekeleza hadidu ya rejea itakayowawezesha  kuwabaini waliohusika katika kupanga, kufadhili, kuratibu na kufanya ghasia wakati na baada ya uchaguzi huo.

Amefafanua kuwa katika uchunguzi wa awali, Tume ilijikita katika malalamiko kuhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi, watu kupigwa risasi za moto nje ya maeneo ya ghasia, kupotea kwa watu na wengine kupata majeraha makubwa. 

“Pia Tume ilichunguza malalamiko kuhusu watoto, watu wenye ulemavu na wenye hali mbalimbali za kiafya walioathirika na vurugu hizo, pamoja na madai ya kutofuatwa kwa taratibu za kisheria wakati wa kudhibiti ghasia,” alisema Jaji Lila.

Jaji Lila ametoa wito kwa wananchi na taasisi zenye taarifa au vielelezo vinavyoweza kusaidia uchunguzi zinaweza kuviwasilisha katika tume hiyo.