Tanzania imewasilisha mafanikio na hatua zilizochukuliwa kuimarisha haki za binadamu, ikiwemo mageuzi katika sekta ya sheria, demokrasia, utawala bora na usawa wa kijinsia.
Hatua hizo zimewasilishwa Novemba 5, 2026, katika Kikao cha Nne cha Tathmini ya Hali ya Haki za Binadamu kwa Mataifa (UPR), kinachofanyika katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa jijini Geneva, Uswisi.
Katika tathmini iliyopita ya mwaka 2021, Tanzania ilipokea mapendekezo 252 kutoka nchi mbalimbali, ambapo ilikubali 187, yakiwemo 20 kwa sehemu, na kukataa 65.
Mapendekezo yaliyokubaliwa yamekuwa msingi wa mageuzi yaliyotekelezwa.
Katika upatikanaji wa haki, Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imewafikia wananchi milioni 7.9, wakiwemo wanawake zaidi ya milioni nne. Serikali pia imetafsiri sheria 446 kwa Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kuelewa haki na wajibu wao.
Aidha, Tanzania Bara imepunguza mrundikano wa mashauri mahakamani kutoka asilimia 10 hadi tano, huku muda wa wastani wa kumaliza mashauri ukishuka kutoka siku 95 hadi 66.
Kwa upande wa Zanzibar, mrundikano wa mashauri umepungua kutoka asilimia 43 hadi 18, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha upatikanaji wa haki nchini.
