Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amesema maendeleo ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Makutupora–Tabora ni mazuri, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili kufidia muda uliopotea kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji.
Amesema hayo leo Jumamosi Novemba 07, 2026 Tura mkoani Tabora wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, ambapo amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wake ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.
Amesisitiza kuwa kukamilika kwa vipande vyote vya mradi huo, hususan kipande cha tatu na nne, ni muhimu katika kufanikisha malengo ya jumla ya ujenzi wa reli hiyo, akieleza kuwa kutokamilika kwake kutazuia mradi kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Sambamba na hayo, amesisitiza kuwa, Wizara ya Fedha na Wizara ya Uchukuzi zitaendelea kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha upatikanaji wa fedha na usimamizi wa utekelezaji wa mradi huo unakwenda sambamba, ili kuondoa vikwazo vinavyoweza kuchelewesha ujenzi na kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi katika utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa kuzingatia malengo na ratiba iliyowekwa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Machibya Shiwa, ameeleza hatua zinazochukuliwa na shirika hilo kusimamia utekelezaji wa mradi na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa mradi, Salim Omary Salim
ameeleza kuwa, usimamizi wa utekelezaji unaendelea kufanyika kwa kuzingatia masharti ya kimkataba, viwango vya ubora na matakwa ya kimazingira ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa.
