Rais Samia Suluhu Hassan, amewataka Watanzania kuimarisha amani, utulivu wakati kuelekea michuano ya Kombe la Mataifa Africa (AFCON 2027) itakayofanyika Tanzania, Kenya na Uganda.
Rais Samia ameeleza hayo leo Alhamisi Novemba 19,2026 wakati akiwasalimia wananchi wa Jiji la Arusha muda mchache baada ya kuwasili katika mkoani humo kwa ziara ya kikazi.
Mkuu huyo wa nchi, amesema kupitia michuano ya AFCON 2027 Taifa litapata ugeni wa mataifa mbalimbali watakaofika Arusha na Tanzania kwa ujumla, akiwataka pia kuimarisha usafi wa mazingira.
“Kwa sababu wageni watataka kwenda Ngorongoro na maeneo mbalimbali ya Arusha, la kwanza ndugu zangu amani na utulivu wa Arusha yetu na nchi yetu. Tukiwa salama wageni watakuja na kucheza salama,” amesema Dkt Samia.
Mbali na hilo, Rais Samia amesema ujio wa AFCON 2027 ni fursa kiuchumi kuanzia wafanyabiashara wadogo hadi wamiliki wa hoteli, akieleza kuwa fedha itatembea.
