You are currently viewing Mwigulu aagiza ujenzi barabara za Mahenge, Malinyi uanze

Mwigulu aagiza ujenzi barabara za Mahenge, Malinyi uanze

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ameiagiza Wizara ya Ujenzi iharakishe taratibu za kumpata mkandarasi wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Lupiro–Mahenge, yenye urefu wa takribani kilometa 42 huku akielekeza kutathminiwa uwezekano wa kuanza na maeneo korofi yanayohatarisha usalama wa wananchi.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumanne, Novemba 24, 2026) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mapinduzi, Mahenge, wilayani Ulanga, mkoani Morogoro.

Alisema Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo katika shughuli za kiuchumi na hivyo Wizara ya Ujenzi inapaswa kuharakisha taratibu za utekelezaji wa mradi huo.

“Siyo kwamba barabara yenu ilipuuzwa, la hasha. Umuhimu wa barabara yenu unatambulika. Ninyi ni wilaya ya uzalishaji, ni wilaya ya kiuchumi. Ninyi hamhitaji barabara kwa ajili ya matembezi tu. Hii ni barabara ya kiuchumi, tena uchumi wa nchi nzima,” alisema.

Waziri Mkuu aliielekeza Wizara hiyo ishirikiane na taasisi zake kutafuta mkandarasi, huku ikiangalia uwezekano wa kuanza ujenzi katika maeneo yenye changamoto kubwa zaidi za usafiri. “Kwa sababu ipo kwenye bajeti, Mheshimiwa Waziri, ongea na makao makuu, ongea na taasisi zetu, tafuteni mkandarasi. Ikiwezekana busara itumike hii ya kuanza na eneo korofi zaidi,” alisema.

Alisema hatua hiyo itasaidia kukabili changamoto za usafiri katika maeneo hatarishi wakati Serikali ikiendelea na taratibu za ujenzi wa barabara nzima.

Akitoa ufafanuzi kuhusu barabara hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alisema mradi huo umefanyiwa usanifu na umejumuishwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027.

Alisema eneo la Mlima Ndororo ni miongoni mwa sehemu zenye changamoto kubwa za usafiri ambazo zinaweza kupewa kipaumbele katika utekelezaji wa mradi huo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwaagiza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga wahakikishe wakulima hawatozwi ushuru wanaposafirisha mazao kutoka mashambani kwenda nyumbani. “Msitoze ushuru mazao yanapotoka shambani, tozeni yanapofanyiwa biashara,” alisema.

Alitoa agizo hilo baada ya mmoja wa wananchi kulalamikia kuwepo kwa mageti mengi ya ukusanyaji wa ushuru, akieleza kuwa wakulima wanatozwa ushuru wanapotoa mazao mashambani na wanapoyasafirisha kwenda kwenye mashine za uchakataji.

Dkt. Mwigulu aliwataka Mwenyekiti wa Halmashauri, madiwani na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga wapitie sheria ndogo za ukusanyaji wa ushuru ili kuondoa usumbufu kwa wakulima. “Mtu akiwa ametoka kuvuna anapeleka nyumbani kwake hatozwi ushuru. Wanaofanya biashara huko ndiko ambako kuna utaratibu huo,” alisisitiza.

Mapema mchana, akizungumza na wakazi wa Malinyi, Dkt. Mwigulu alisema kuchelewa kwa ujenzi wa barabara ya Ifakara–Malinyi kulitokana na Serikali kuelekeza fedha katika kukamilisha Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere hali iliyoathiri mtiririko wa fedha kwa baadhi ya miradi mingine.

Waziri Mkuu alisema kuwa Serikali imepanga kushughulikia miradi ya barabara kwa makundi matatu, ikianza na miradi ambayo wakandarasi waliondoa mitambo kutokana na kutolipwa, ikifuatiwa na ile ambayo mikataba ilishasainiwa lakini malipo ya awali hayajatolewa, na hatimaye miradi mipya inayosubiri hatua za mikataba.

“Barabara ya Ifakara–Malinyi ipo katika kundi la pili, ambapo mkandarasi ameshapatikana na kinachosubiriwa ni malipo ya awali ili ujenzi uanze. Barabara hii ni barabara ya kiuchumi, ni barabara ya uzalishaji,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Kasekenya, alisema Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa kilometa 112 za barabara hiyo, kuanzia Ifakara kuelekea Mtimbira, na Wizara imewasilisha maombi ya fedha Hazina kwa ajili ya kuanza utekelezaji.

Dkt. Mwigulu alisema ataendelea kufuatilia ujenzi wa barabara hizo kutokana na umuhimu wake katika usafiri, usafirishaji wa mazao na shughuli za kiuchumi za wananchi.