You are currently viewing Aweso aitaka DAWASA kushirikiana na wenyeviti mitaa kutatua changamoto za maji

Aweso aitaka DAWASA kushirikiana na wenyeviti mitaa kutatua changamoto za maji

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA) kushirikiana kwa karibu na wenyeviti wa mitaa ili kuweza kutatua changamoto za maji pamoja na kurahisisha ufikishaji wa huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo.

Aweso ameyasema hayo leo Februari 18, akizungumza na Wenyeviti wa Mitaa wa Wilaya ya Kinondoni na kuwataka viongozi wa mamlaka hiyo kuhakikisha kila wakati wanashiriki mikutano inayofanywa na wenyeviti hao ili kuweza kusikiliza na kutatua changamoto zilizopo katika maeneo yao.

“Muwape ushirikiano muwe na mawasiliano yao wakipiga simu muwape taarifa wakiwaita wana mkutano mtu wa maji awepo naomba sana mtu wa DAWASA awepo asikilize muweze kutatua changamoto zilizopo kwenye hayo maeneo”

Aidha, Aweso ameitaka mamlaka hiyo kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa za haraka hasa za hitilafu na matengenezo ili kuepuka kutokea kwa sintofahamu na upotoshaji wa taarifa.

Pamoja na hayo Waziri Aweso ameipongeza DAWASA kuwa wa kwanza kutekeleza agizo alilotoa la kuwataka viongozi wa mamlaka za maji nchini kukutana na Wenyeviti wa mitaa na kushirikiana nao ili kutatua changamoto cha maji na kutekeleza miradi ya maji nchini.

Aidha, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Dar Es Salaam(DAWASA), Mhandisi Mkama Bwire amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan  kwa kusaidia upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Kinondoni kufikia asilimia 97%.

Akizungumza katika kikao kazi hicho, Mhandisi Bwire ameeleza kuwa mpaka sasa usambazaji wa maji kwa jiji la Dar Es Salaam umefikia asilimia 93% huku kwa Wilaya ya Kinondoni ikiwa ni asilimia 97%.

“Kinondoni ina kata 20 mitaa 126 tumefika kwenye mitaa yote lakini kazi inaendelea. Serikali imefanya kazi yake ya kupeleka mtandao wa mabomba kwa 97% kuna kazi ya pili ya kuhakikisha ambapo sasa mtandao umefika watu wanajiunganisha kwenye mtandao huo” amesema Mhandisi Bwire.

Mhandisi Bwire ameeleza kuwa mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na Wenyeviti wa mitaa ili kuhakikisha wananchi wanaunganishwa na huduma ya maji safi na salama.

Leave a Reply