Barabara kuu ya Tanga–Segera inatarajiwa kufungwa kwa saa nne leo Oktoba 20, 2026, kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa sita mchana, ili kupisha matengenezo ya dharura katika madaraja ya Hale na Maguzoni yaliyoathiriwa na mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, Mhandisi Msama Msama, amesema matengenezo hayo yanalenga kurekebisha maeneo yaliyoharibiwa na maji ya mvua pamoja na kuimarisha hali ya madaraja hayo ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara hiyo.
Amesema barabara ya Tanga–Segera ni kiungo muhimu kinachounganisha Mkoa wa Tanga na maeneo mengine ya nchi, hivyo matengenezo hayo ni muhimu katika kuimarisha usalama wa usafiri na usafirishaji. Watumiaji wa barabara hiyo wanashauriwa kuzingatia muda wa kufungwa kwake na kupanga safari zao mapema ili kuepuka usumbufu.
