Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imepanga kutekeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mlandizi hadi Ruvu kwenye Stesheni ya SGR kwa awamu, ambapo mkataba wa ujenzi sehemu ya Mlandizi hadi makutano ya Stesheni ya SGR ya Ruvu (Km 15) ulisainiwa Mei 2, 2025 na mkandarasi yupo kwenye hatua za awali za kuanza kazi.
Hayo yamesemwa leo Jumanne bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya wakati akijibu swali la Mbunge wa Kibaha Vijijini mkoani Pwani, Michael Mwakamo aliyetaka kujua ni lini Serikali itaanza ujenzi huo.
Aidha, amesema kwa sehemu ya makutano ya Ruvu hadi Stesheni ya SGR (Km 8) maandalizi ya usanifu yanaendelea na kazi ya usanifu inategemewa kuchukua muda wa miezi mitatu ambapo baada ya usanifu kukamilika, zabuni za ujenzi zitatangazwa.