BEI za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa kipindi cha mwezi Julai zimeshuka hatua inaleta ahueni kwa watumiaji wa bidhaa hizo za mafuta.
Bei kikomo za mafuta zitakazotumika Julai mwaka huu zinaonesha, petroli inayopitia bandari ya Dar es Salaam imepungua kwa Sh96, dizeli kwa Sh151 na mafuta ya taa kwa Sh242.
Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) iliyotangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli zitakazotumika kuanzia leo Jumatano ya Julai Mosi, 2026.
Kupungua kwa bei hiyo sasa itafanya petroli ndani ya Dar es Salaam, lita moja kununuliwa kwa Sh3,990 kutoka Sh4,086 iliyokuwa ikitumika Juni mwaka huu, huku Dizeli ikinunuliwa kwa Sh4,182 kutoka Sh4,333.
Upande wa watumiaji wa mafuta ya taa yanayopitia bandari hiyo watanunua lita moja kwa Sh4,443 kutoka Sh4,685 iliyokuwa ikitumika Juni mwaka huu.
Kwa upande wa watumiaji wa mafuta yanayopitia bandari ya Tanga, sasa watanunua lita moja ya petroli kwa Sh4,051 ikiwa ni pungufu kutoka Sh4,157 huku dizeli ikinunuliwa kwa Sh4,243 kutoka Sh4,404 iliyokuwapo mwezi uliotangulia.
