You are currently viewing Benki TCB yazindua Lipa Popote kurahisisha malipo kwa wafanyabiashara

Benki TCB yazindua Lipa Popote kurahisisha malipo kwa wafanyabiashara

Benki ya Biashara Tanzania (TCB) inajivunia kutangaza uzinduzi wa bidhaa ya LIPA POPOTE, suluhisho la malipo lililobuniwa ili kurahisisha miamala kwa wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) na wamiliki wa biashara. 

Bidhaa hiyo mpya inawawezesha wateja wa Benki ya TCB kupokea malipo moja kwa moja kwenye akaunti zao za benki kupitia namba moja ya mfanyabiashara iitwayo LIPA POPOTE. 

Aidha, wenye akaunti katika Benki ya TCB wataweza kulipia bidhaa na huduma kwa urahisi wakitumia namba maalum ya muuzaji (Till Number), hivyo kufanya miamala iwe rahisi zaidi kuliko hapo awali.

Akifafanua kuhusu bidhaa hiyo, Afisa Mkuu wa Huduma za Kidijitali na Ubunifu wa Benki ya TCB, Jesse Jackson alisema LIPA POPOTE imebuniwa kushughulikia hitaji la malipo ya kifedha linaloongezeka kwa kasi nchini miongoni mwa wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) ambao ni uti mgongo wa uchumi wa taifa. 

Alisema suluhisho hilo linalenga kurahisisha mchakato ya malipo kwa wamiliki wa biashara, kuwawezesha kupokea malipo papo hapo na kwa usalama.

Alisema bila kuhitaji gharama za usajili, huduma hii inapatikana kirahisi, ikiongeza wigo wa ujumuishi wa kifedha kwa kuondoa vizuizi vya miamala ya kidijitali kwa biashara mbalimbali kote nchini.

“TCB tumekusudia kukuza ubunifu unaogusa maisha ya Watanzania. LIPA POPOTE inadhihirisha dhamira yetu ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) kwa kutoa suluhisho bora kwa malipo rahisi na salama.

LIPA POPOTE ni zaidi ya njia ya malipo; ni hatua kuelekea uwezeshaji wa kiuchumi kwa wafanyabiashara nchini, kuanzia mijini hadi jamii za vijijini. Lengo letu ni kuzifanya huduma za kifedha ziwe salama, nafuu na zipatikane kwa watu wote,” alisisitiza Jackson.

Naye Mkurugenzi wa Biashara kwa Wateja Wadogo na wa Kati – TCB,Lilian Mtali alisema kwa kuzindua suluhisho la kidijitali la malipo kama vile LIPA POPOTE, wanaboresha kikamilifu malengo ya Tanzania ya kuongeza ujumuishi wa kifedha kwa wafanyabiashara, watu binafsi na jamii ambazo hazijafikiwa:

“Njia hii ya malipo inatarajiwa kubadilisha namna biashara ndogo zinavyofanya kazi, na kurahisisha miamala ya kifedha.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya Tanzania, Adam Mihayo alisema wanashuhudia mageuzi ya kidijitali yanayoendelea kuboresha uchumi kila kukicha.

Alisema TCB inalenga kuwa mstari wa mbele katika kutoa masuluhisho ya kibenki yenye ubunifu na kuchochea ujumuishi wa kifedha kwa wote. “LIPA POPOTE ni uthibitisho wa dhumuni letu la uwezeshaji uchumi na upatikanaji wa huduma za kifedha, ili kuwanufaisha Watanzania wote na huduma za kisasa za kibenki,” alisema.

Leave a Reply